WATU WATANO wameuwawa na zaidi ya 20 kujeruhiwa kwenye klabu ya starehe mjini Garissa, kaskazini-mashariki mwa Kenya.
Washambuliaji walirusha maguruneti kwenye klabu hiyo na kisha kuwapiga risasi watu waliojaribu kukimbia.
Mji wa Garissa uko karibu na mpaka wa Somalia ambako jeshi la Kenya lilingia mwezi wa Oktoba, kuwaandama wapiganaji wa al-Shabaab.
Polisi wanasema watu waliohusika na al-Shabaab huenda walifanya shambulio hilo.
Na katika hotuba yake ya kukaribisha mwaka mpya, Rais Kibaki wa Kenya amezungumza juu ya wanajeshi wa nchi yake walioko Somalia.
Amesema ” Kenya inakusudia kumaliza kazi iliyoanza.
Tuna jukumu kwa watu wetu na watu wa Somalia ambao hawakuona amani kwa muda wa miaka 20.
Raia hao wanatumai kufikia amani na ustawi wa taifa lao.
Amani ya Somalia ni msingi muhimu katika kukamilisha amani na ustawi wa Pembe ya Afrika na Afrika Mashariki.”
Akigusia juu ya uchaguzi wa mwisho wa mwaka 2012, Rais Kibaki alisema nchi itapita kwenye kipindi cha kubadilisha uongozi na kugawa madaraka kutoka serikali, na kuutawanya kwenye serikali za majimbo.
Alisistiza kuwa wananchi watambue kuwa Kenya ni muhimu zaidi kushinda masilahi ya mtu mmoja.
“Lazima tuchukue hatua kuhakikisha kuwa tunabaki wamoja” alisema Rais Kibaki.
-BBC