Na Janeth Mushi, Arusha
KESI ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema (CHADEMA) inayoendelea kusikilizwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, kesho inaingia hatua nyingine kwa mdai wa pili kutoa ushahidi.
Wiki iliyopita shahidi wa kwanza Musa Mkanga alitoa ushahidi wake akiongozwa na wakili anayewawakilisha Alute Mughwai, kufuatiwa mahojiano kutoka kwa mawakili wa wajibu maombi Method Kimomogoro anayemtetea Lema na Timon Vitalis anayemtetea Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Wadai katika kesi hiyo namba 13 ya 2010 ni Musa Mkanga, Happy Kivuyo na Agness Mollel ambao kwa pamoja wanaiomba mahakama kutengua matokeo ya uchaguzi kwa madai kuwa Lema alikiuka taratibu, kanuni na Sheria ya Uchaguzi Mkuu wa 2010. Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Sumbawanga, Gabriel Rwakibarila ndiye anayesikiliza kesi hiyo baada ya Jaji Aloyce Mujulizi aliyekuwa anasikiliza kujiondoa.
Jaji huyo amepiga marufuku mtu yeyote kuandika mwenendo wa kesi hiyo, mahakamani hapo isipokuwa waandishi wa habari pekee huku akiagiza watumishi wa mahakama kuhakikisha wanatenga viti kwa ajili ya wanahabari ili waweze kufanya kazi zao wakiwa wamekaa.
Jaji Rwakibarila alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki baada ya kuona
baadhi ya waandishi wa habari wanaoripoti mwenendo wa kesi hiyo
wakiwa wamesisima; “Nataka siku nyingine waandishi wa habari wapewa viti vyao maalum na ikiwezekana sehemu hii ya mbele na hakuna mtu mwingine yeyote anayeruhusiwa kuandika akiwa humu mahakamani,” alisema Jaji huyo.
Aidha kesi hiyo ambayo imeanza kusikilizwa mfululizo wiki iliyopita, imekuwa ikivuta idadi kubwa ya watu Mahakamani hapo, hali
inayosababisha waandishi kukosa mahali pa kukaa wanapokuwa
wakifuatilia shauri hilo.
Wanahabari mkoani hapa wameupongeza uamuzi wa Jaji Rwakibarika kwa kutambua umuhimu wa sekta hiyo ya habari na kutaka mfano huo uingwekatika nyanja nyingine za serikali.