Na Mwandishi wetu, Arusha
SHAHIDI wa pili wa upande wa walalamikaji katika shauri la kupinga matokeo ya uchaguzi wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), Agness Mollel ameileza mahakama kuwa aliyekuwa mgombea wa nafasi hiyo kupitia CCM Dk. Batilda Buriani alidhalilishwa kijinsia na Lema baada ya kudai kuwaeleza wapiga kura kuwa wasimpigie kura kwa kuwa hafai kuwa kiongozi huku akidai alikuwa na mimba ya Mbunge wa Monduli Edward Lowassa.
Shahidi huyo alitoa madai hayo jana Mahakama Kuu Kanda ya Arusha inayosikiliza kesi hiyo, ambapo ameileza Mahakama kuwa, Lema alisema iwapo Dk. Batilda angechaguliwa jimbo hilo lingekuwa limeuzwa Monduli.
“Msimchague huyu mwanamke Dk. Batilda kwa sababu ameolewa Zanzibar na hapo alipo ana mimba ya Lowassa hivyo mkimchagua jimbo hili mtakuwa mmeliuza kwa Lowassa na pia mwanamke huyo alisema kuwa ataifunga Redio Safina na kufungua msikiti,” alidai Shahidi huyo, akimnukuu Lema katika moja ya mikutano yake ya kampeni
Agness alisema hayo jana wakati alipokuwa akiongozwa na wakili anayemwakilisha Alute Mughwai katika shauri hilo, ambapo alidai kuwa Lema aliyasema hayo Septemba 1 mwaka 2010 katika eneo la Bigsister, kata ya Olerien katika mkutano wa hadhara wa kampeni.
Shahidi huyo alidai mahakamani hapo kuwa baada ya kusikia maneno hayo yaliyotolewa na Lema dhidi ya mgombea wa CCM, hakuweza kuvumilia ilibidi aondoke katika mkutano huo akidai kuumizwa na maneno hayo kijinsia, kidini na kikabila.
Kwa upande wake wakili wa Mdaiwa wa kwanza katika kesi hiyo (Lema) Method Kimomogoro, akimohoji shahidi huyo alimwuliza kuhusu hati yao ya madai, na mahojiano yao yalikuwa kama ifuatavyo:
Wakili: Agness unakumbuka umesaini kwenye hati mliyofungulia kesi hii, maneno uliyosema uliyashuhudia?
Shahidi: Ndiyo nakumbuka
Wakili: Maelezo uliyoandika katika hati hiyo, ulisema kuwa Lema alisema Dk. Batilda asichaguliwe kwa sababu ni mwanamke na hafai kuwa kiongozi wa kuchaguliwa, na maneno hayo umesaini kuwa uliyasikia katika eneo la fantastic, Olmatejoo Kata ya Olorien?
Shahidi: Si kweli.
Katika hati hiyo iliyopo mahkamani, shahidi huyo pamoja na kusaini hati hiyo chini yab maelezo aliyayatoa, alikiri saini ni yake ila alipingana na maneno hayo.
Wakili:Ukiikana maneno yaliyopo kwenye hati yako kwa kusema ulichoandika si ya kweli, jaji atalazimika kuifuta, hivyo ieleze mahakama ni kweli uliyashuhudia maneno unayodai yamesemwa na Lema katika eneo la Olmatejoo au Bigsister? alihoji
Shahidi: Nimeshuhudia ya Ol Matejoo
Wakili: Kwa hiyo kama mtu atakuja kusema ulihudhuria mkutano wa tarehe 22.9.2010 eneo la Fantastic, Elerai, atakuwa mwongo?
Shahidi: Atakuwa mwongo maana hata eneo hilo silifahamu
Wakili: Unakumbuaka kwenye hati hii ambayo sijui umeikana au vipi, ambayo mmeambatanisha barua aliyoaondika Dk. Batilda kwa msimamizi wa uchaguzi ya kulalamika kuhusu kauli za Lema,inawezekana hukuisoma, je hukusomewa?
Shahidi: Sikuosoma wala kusomewa
Wakili: Nani alikuburuza kukuleta kwenye kitu usichokijua vizuri, hizi barua ulizoambatanisha kwenye hati umesema hukuisoma uliburuzwa na nani? Shahidi Hapana sikuburuzwa
Wakili: Ulikuwa na tape ya kunasa hayo maneno au kalamu?
Shahidi: Sikuwa nayo, nilikuwa msikilizaji tu
Kimomogolo alimuhoji shaidi huyo iwapo aliwahi kumweleza Dk. Batilda kuhusu maneno aliyoyasikia kutoka kwenye mkutano?
Shahidi: Nilimweleza siku ya pili baada ya mkutano ule
Wakili: Hayo maneno kama yalitamkwa kweli, yalimgusa Batilda wewe binafsi hayo maneno yalikusababishia madhara gani?
Shahidi:Yaliniumiza kijinsia, kidini na ukabila.
Katika shauri hilo namba 13 la mwaka 2010 wadai katika kesi hiyo ni Musa Mkanga, Happy Kivuyo na Agness Mollel ambao kwa pamoja wanaiomba mahakama kutengua matokeo ya uchaguzi kwa madai kuwa Lema alikiuka taratibu, kanuni na Sheria ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31,2010, huku Timon Vitalis akimtetea Mwanasheria Mkuu wa Serikali.