Na Ally Daud – Maelezo
SERIKALI imetoa wito kwa wananchi kuacha matumizi mabaya ya vyandarua ili kusaidia jitihada za Serikali katika kupambana na ugonjwa wa Malaria nchini. Akizungumza Jijini Dar es salaam katika Uzinduzi wa Utafiti wa Matokeo ya Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria wa Mwaka 2015/16, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Mpoki Ulisubisya amesema kuwa kumekuwepo na tabia ya wananchi kutumia vyandarua wanavyopewa na Serikali kwa matumizi yasiyo sahihi kama kuvulia samaki, kuwekea wigo mifugo na kuzungushia wigo bustani.
“Watu wengi wamekuwa wakitumia vyandarua vinavyotolewa na Serikali kwa matumizi yasiyo sahihi badala ya kujikinga na Mbu waenezao malaria. Hii ni kutokana na utafiti huu kuonyesha kuwa asilimia 14 ya watoto wa chini ya miaka 5 ambao walipimwa Malaria kwa kutumia kipimo cha kutoa matokeo kwa haraka yaani Rapid Diagnostic Tests (RDT) walikuwa na Malaria,” amesema Dkt. Ulisubisya.
Aidha amesema kuwa kiwango cha maambukizi ya Malaria bado ni kikubwa ikilinganishwa na kiwango kilichopatikana wakati wa Utafiti wa UKIMWI na Malaria wa Mwaka 2011-12 hivyo ni vyema jamii ikaendelea kupambana na ugonjwa huu kwani bado ni tishio kwa watoto na Wananchi kwa ujumla. Dk. Ulisubisya amesema kuzinduliwa kwa Matokeo haya kutasaidia Serikali kuboresha huduma za afya kwa kuyafanyia marekebisho mapungufu yaliyopo katika utoaji wa huduma za malaria nchini.
Akizungmzia huduma za afya kwa akinamama wajawazito, Dk. Ulisubisya amesema utafiti umeonyesha kuwa kiwango cha akina mama wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma ya afya, kutoka asilimia 51 mwaka 2010 kufikia asilimia 60 mwaka 2015 na kuongezeka kwa kiwango cha akina mama wanaosaidiwa na wataalam waliosomea wakati wa kujifungua kutoka asilimia 50 kufikia asilimia 60 mwaka 20015/16.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Kitakwimu, Mr. Irenius Ruyobya amesema kuwa utafiti huu ni wa muhimu sana katika kuboresha huduma za afya hasa katika kupambana na Malaria.
Amesema ili Serikali iweze kuboresha huduma za afya na kupambana na Malaria, takwimu hizi ambazo zimezinduliwa leo zitasaidia Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa afya katika kupanga, kutekeleza na kupima utekelezaji wa miradi mbalimbali ya afya nchini.
Mr. Ruyobya amesema utafiti huu ni wa sita kufanyika nchini ambapo kwa mara ya kwanza ulifanyika mwaka 1991 na kufuatiwa na utafiti wa mwaka 1996, 1999, 2004/5 na 2010.