Na Thomas Dominick, wa Habari Motomoto, Musoma
SERIKALI imeagiza Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za miji, Wilaya na mawakala zinazotoa huduma kwa watu wenye ulemavu kuweka mipango madhubuti ya haki za watu wenye ulemavu kuimarisha mahusiano yaliyopo kati ya vyama vya watu wenye ulemavu na watendaji.
Akisoma hotuba ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Mkuu wa Mkoa wa Mara John Tuppa Siku ya maadhimisho ya watu wenye ulemavu Duniani ambapo kitaifa ilifanyika Mkoani hapo, alisema kuwa serikali kuu inaendelea kutangua madaraka kwenda ngazi ya serikali za mitaa ili kusogeza huduma za ustawi wa jamii.
“Hatua hii itawezesha Halmashauri zote nchini kusimamia na kutekeleza huduma za watu wenye ulemavu, hivyo serikali, asasi zisizo za kiserikali na watu binafsi zishiriki katika kuhakikisha kwamba juhudi za makusudi zinafanywa ili kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu,” alisema Tuppa.
Alisema kuwa serikali itaendelea kusimamia upatikanaji wa taarifa za mifumo isiyo rasmi kwa watu wenye ulemavu hususani viziwi kwa kuhakikisha kuwa katika vyombo vya habari kupitia luninga kuhakikisha mkalimani wa lugha za alama ili waweze kupata taarifa muhimu zinazotolewa kwa manufaa ya maendeleo ya nchi na ustawi wa jamii kwa ujumla.
“Serikali itaendelea kuboresha miundo mbinu kwa watu wenye ulemavu ikiwa ni majengo yanayotoa huduma kwa umma kutofikika na kusababisha walemavu kushindwa kupata huduma muafaka na wanazostahili,” alisema.
Alisema kuwa Serikali kupitia kitengo cha michoro na ramani wameandaa mwongozo wa ramani za majengo ya umma hivyo kabla ya kufanya ujenzi wowote lazima ramani ikaguliwe ili kuona kama imekidhi mahitaji hayo.
Tuppa alisema kuwa Serikali kupitia wizara ya afya na ustawi wa jamii inatenga fedha kila mwaka ili kuviongezea uwezo vyama hivyo na suala la kutotosheleza kwa ruzuku linatokana na uwezo wa serikali kifedha na majukumu yanayohusiana na huduma katika sekta mbalimbali.
Alisema kuwa suala la watu wenye ulemavu ni mtambuka ambalo linamgusa kila mmoja na kila wizara inatakiwa kuwa na dawati la kuratibu masuala la watu wenye ulemavu kwa kushitikiana pamoja na wizara ya afya na ustawi wa jamii yenye dhamana juu ya masuala ya watu wenye ulemavu nchini.