Frank Mvungi – Maelezo
SERIKALI imewataka wananchi kujihadhari na makampuni yanayojiingiza katika kazi za upimaji ardhi au uthamini bila ya kusajiliwa na bodi au halmashauri zenye mamlaka ya kusimamia taaluma husika. Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Justo Lyamuya wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliolenga kutoa utaratibu unaotakiwa kufuatwa na wananchi katika upimaji ardhi.
“Hadi sasa wapima ardhi waliosajiliwa ni 290 wakati makampuni yaliyosajiliwa na Baraza la Taifa la wapima na wathamini ardhi ni 58 hivyo hakuna haja ya wananchi kutapeliwa na vishoka,” alisema Lyamuya.
Akifafanua Lyamuya amesema kuwa ni vyema wananchi wakatumia makampuni yaliyosajiliwa kufanya kazi ya kupima ardhi ili kuepuka migogoro ambayo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na ukiukwakwaji wa sheria na taratibu za upimaji ardhi.
Akifafanua kuhusu wathamini (valuers) Lyamuya alisema hadi sasa wataalamu waliosajiliwa ni 320 na makampuni yalisajiliwa na Baraza ni 54. Pia Lyamuya alisema kuwa kazi za upimaji viwanja zitakazo wasilishwa Wizarani ambazo hazikufuata taratibu na kwa mujibu wa sheria ya upimaji Ardhi sura 324 ya mwaka 1957 hazitapokelewa.
Pia mambo yanayopaswa kuzingatiwa katika upimaji wa ardhi (mashamba na viwanja) lyamuya amesema upimaji usiozingatia ushirikishwaji na kutambua mipaka kwa maridhiano hautapokelewa.
Aidha makampuni ya upimaji yanayowasilisha kazi za upimaji kwa Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani ambazo hawakuzisimamia wao wenyewe au wawakilishi wao na kudhibitika; kazi hizo hazitapokelewa na kwa mujibu wa sheria za kusajili makampuni ya upimaji Na. 2 ya mwaka 1977 yataadhibiwa ikiwa ni pamoja na kusimamishwa.
Halmashuri ya Taifa ya wapima Ardhi ni chombo cha Serikali kilichoundwa kwa mujibu wa sheria Na. 2 ya mwaka 1977, Jukumu kubwa la chombo hiki ni kufanya usajili wa wataalam wapima Ardhi, kusimamia weledi wa taaluma na mwenendo wa utendaji katika masuala ya kupima ardhi (Land Survey) kuthamini mali (property valuation) na kuendeleza ardhi (estate management).