Serikali yawaonya wanaouza ardhi kwa wawekezaji

Naibu wa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi nchini, Gooluck Ole Medeye.


Veronica Kazimoto na Aron Msigwa, Dodoma
20/6/2011

SERIKALI imewataka wananchi kulinda na kuhifadhi ardhi zao na kuacha tabia ya kuziuza holela kwa wawekezaji bila kufuata kanuni na matakwa ya sheria ya Ardhi.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi Ole Medeye wakati akijibu swali la mbunge wa Mufindi Kusini Mhe. Medrad Lutengano Kigola aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na serikali kufuatia vitendo vya baadhi ya wananchi kuporwa maeneo ya kilimo na Wawekezaji.

Amesema kuna tabia ya baadhi ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini wanaojihusisha na uuzaji wa ardhi kwa wawekezaji bila kufuata utaratibu huku akiyataja maeneo ya jimbo la mufindi kusini ya Isaula, Kiyowela, Rugema, Mkalala, Kihanga na Magunguli ambapo wenye viwanda vidogo na wawekezaji wa upandaji wa miti huuza ardhi zao na baadaye kulalamika kuwa wameporwa ardhi na wawekezaji.

“Uchunguzi uliofanywa na wizara yangu umebaini kuwa wananchi wengi wa jimbo la mufindi wamepungukiwa na ardhi ya kulima na baadhi yao wamediriki kuvamia maeneo ya wawekezaji wakidai kuwa ni yao suala linalosababisha usumbufu kwa wawekezaji nchini ,” alisisitiza.

Ameongeza kuwa hivi sasa tabia ya wananchi kuuza ardhi kwa kudanganyika na fedha kidogo wanayopewa na wawekezaji imeenea katika sehemu mbalimbali na kutahadharisha kuwa hali hiyo inasababisha wananchi wengi kubaki mafukara baada ya kumaliza fedha za mauzo.

“ Kwa kutambua tabia hii na serikali kuliona hili, wizara yangu inaendelea kutoa elimu kwa viongozi wa serikali za mitaa na wananchi kwa ujumla ili kuhakikisha kuwa ardhi haitolewi hovyo kwa wawekezaji bila kufuata utaratibu na matakwa ya sheria ya ardhi” Amesisitiza.

Hata hivyo Ole Medeye ametoa wito kwa wabunge, viongozi na watendaji mbalimbali wa serikali kushirikiana na Wizara yake kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi ardhi na kuingia ubia na wawekezaji badala ya kuuza kwa manufaa yao na vizazi vijavyo.

Ikumbukwe kuwa hivi karibuni kumekuwepo ongezeko la migogoro ya ardhi kati ya wananchi na wawekezaji katika maeneo mbalimbali nchini hali inayosababisha uvunjifu wa amani kufuatia wananchi kuvamia maeneo ya wawekezaji na kuharibu mashamba na mali.