Serikali Yawaandalia Neema Wakulima Mauzo ya Mazao

Rais Jakaya Kikwete katika picha ya pamoja na baadhi ya wageni wanaoudhuria mkutano wa mapinduzi ya kijani Arusha.

UKOMBOZI zaidi wa wakulima wa Tanzania utakuja mwishoni mwa mwaka ujao wakati Serikali inapopanga kuzindua Soko la Mazao (Commodity Exchange) ambalo kazi yake kuu itakuwa ni kuwahakikishia soko la uhakika zaidi na bei za uhakika zaidi wakulima.

Dk. Eleni Z. Gabre Madhin ambaye anashauri kuhusu uanzishwaji kwa Soko la Mazao katika Tanzania amemwambia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuwa soko hilo linaweza kuanzishwa mwishoni mwa mwaka ujao, 2013, ili mradi tu mchakato wa kuanzishwa kwake uanze Desemba, mwaka huu.

Rais Kikwete na Dk. Eleni Madhin wamekutana kwenye Hoteli ya Ngurdoto mjini Arusha ambako wote wawili wanahudhuria Mkutano wa Pili wa Taasisi ya Mapinduzi ya Kijani katika Afrika (AGRA) ambao Rais Kikwete ameufungua leo kwenye Ukumbi wa Mikutano ya Kimataifa wa Tanzania kwenye Hoteli ya Ngurdoto.
Dk. Eleni Madhin ambaye ni Mwanzilishi na Mtendaji Mkuu wa Soko la Mazao la Ethiopia ameshauri kuwa Kikosi kazi cha kuanzishwa kwa Soko hili kianzishwe haraka iwezekanavyo ili kuwezesha mchakato wa kuanzishwa kwa Soko hili uweze kuanza Desemba, mwaka huu.

“Kama tukianza mchakato Desemba, mwaka huu, na tukiweza kuunda Kikosi kazi katika wiki chache zijazo, basi naweza kukuhakikishia Mheshimiwa Rais kuwa utaweza kuwa na Soko la Mazao linalofanya kazi mwishoni mwa mwaka 2013,” amesema Dk. Eleni Madhin na kuongeza:

“Ushauri wangu ni kwamba Mheshimiwa Rais ukubali kuanzisha Kikosi kazi cha Taifa kikishirikisha maofisa kutoka taasisi mbali mbali zikiwamo Wizara ya Kilimo, Wizara ya Fedha, Wizara ya Biashara na Viwanda, Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA), Mamlaka ya Soko la Mitaji…na taasisi nyingine ambazo unaona zinafaa ili kazi hii ianze mapema iwezekanavyo.”

Rais Kikwete pia amekutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mbolea ya Yara, Bwana Jorgen Ole Haslestad. Viongozi hao wawili wamezungumzia uwekezaji wa Yara katika sekta ya kilimo katika Tanzania.

Aidha, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Shirika la Kimataifa ya Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Dk. Konaye Mwanze. Dk. Mwanze amemwambia Rais Kikwete kuwa Tanzania inatarajiwa kupata msaada wa kati ya dola za Marekani milioni 75 na milioni 80 katika muhula wa kati ya mwaka 2014 na 2017.