WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda amesema Serikali imeamua kuunda timu ya watu 10 kutoka kada tofauti wakiwemo viongozi wa dini ambao watapewa jukumu la kufanya kazi ya usuluhishi kwenye vijiji vyenye migogoro baina ya wafugaji na wakulima wilayani Kiteto mkoani Manyara.
Ametoa kauli hiyo Novemba 23, 2014 wakati akiwasilisha salamu za Serikali kwenye ibada ya kumweka wakfu Askofu wa sita wa Dayosisi ya Central Tanganyika ya Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Dickson Chilongani iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu, mjini Dodoma.
Waziri Mkuu ambaye kwenye ibada hiyo alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete aliyeko nje ya nchi kwa matibabu alisema: “Hali ya Kiteto ni changamoto kama alivyosema Askofu Mkuu, Dk. Chimeledya lakini inahitaji ufumbuzi kutoka kwa wadau tofauti na siyo Serikali peke yake…inataka Serikali, wananchi, vyombo vya dola lakini pia na Kanisa lazima lihusishwe ili kujenga upya maadili ya jamii.
“Ukiwa na kundi kubwa la watu ambao hawamwogopi Mungu ni tatizo. Na hii ndiyo iliyoko kule. Watu wanauana kwa sababu ya hasira, ni hasira gani hiyo inayokufanya usiogope kutoa roho ya mwenzako,” alihoji.
Alisema timu itakayoundwa itapewa jukumu la kufanya usuluhishi na kupata maridhiano (reconciliation) kijiji kwa kijiji huku ikipeleka ujumbe wa amani. “Tunataka kutumia Kiteto kama mradi wa majaribio (pilot project) kwenye suala la kutafuta amani kwenye maeneo kama haya,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema wilaya ya Kiteto inaingiliana na mikoa mitano ambayo ni Tanga (Kilindi), Morogoro (Gairo); Dodoma (Kongwa) Manyara (Simanjiro) na Arusha (Monduli) hali ambayo inachangia kuwepo na muingilianio mkubwa wa kijamii.
Waziri Mkuu alitaja hatua nyingine zitakazochukuliwa na Serikali kuwa ni kupima ardhi inayogombewa yenye ukubwa wa hekta 133,000 na kuigawa kwa wafugaji ili wafuge kwa mtindo wa ranchi na inayobakia igawiwe kwa wakulima. Vilevile, Waziri Mkuu alisema idadi ya vituo vya polisi itaongezwa kwenye miji midogo badala kutegemea kituo kimoja tu cha polisi kilichopo Kibaya.
Alikuwa akijibu hoja iliyotolewa na Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk. Jacob Chimeledya ambaye alisema Serikali ina wajibu wa kulinda maisha ya kila Mtanzania na kutoa mfano wa wilaya ya Kiteto ambako alisema hakuna amani kwa sababu watu wanauana hovyo.
Katika hotuba yake ya kumkaribisha Waziri Mkuu, Askofu Chilongani alisema ameanza kukosa usingizi kutokana suala la umaskini na kukosekana mfumo wa pensheni miongoni mwa wachungaji na makasisi wa kanisa hilo hasa wa vijijini ambao alisema hawana kipto cha uhakika.
“Makasisi na wachungaji hawa wanahudumia Watanzania wote, wanachopata ni kiasi kidogo mno kuweza kuweka kwenye mifuko kama NSSF, bado pia wana mahitaji yao, wanatakiwa wawasomeshe watoto wao…natamani kuwe na mfumo ambao utawawezesha kupata pensheni ili wanapostaafu wajikute hata wana vibanda vya uhakika vya kuishi na familia zao,” alisema na kushangiliwa na mamia ya wachungaji waliohudhuria ibada hiyo.
Akizungumzia kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Dk. Chilongani aliiomba Serikali isimamie zoezi hilo liwe huru na la haki na kuhakikisha linaisha kwa amani. “Niwasihi pia Watanzania wenzangu, wawachague viongozi waadilifu, wasiwachague viongozi ambao wanakimbilia uongozi au wenye kudhani kuwa ubunge au udiwani ni halali yao na siyo dhamana kutoka kwa wananchi,” alisema.