Frank Mvungi – Maelezo
SERIKALI yatumia zaidi ya bilioni 16 kujenga Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (the Law School of Tanzania). Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Msemaji wa Wizara ya Katiba na Sheria, Omega Ngole wakati wa ziara ya waandishi wa habari katika taasisi hiyo iliyolenga kuona hatua iliyofikiwa tangu kuanza kwa ujenzi wake mwaka 2010.
“Baada ya kukamilika kwa ujenzi huu mwaka 2013 uendeshaji wa mafunzo ulihama kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam na kuanza kutumika kwa majengo haya ya kisasa yaliyojengwa na Serikali kupitia Wizara ya Katiba na sheria,”
Akifafanua Ngole amesema ujenzi huo umehusisha ujenzi wa Mahakama ya mafunzo, (Teaching Court) vyumba vya madarasa ( leacture theaters), Maktaba ya Kisasa (Library) Jengo la Utawala (Admistration block) Mgahawa na nyumba za watumishi.
Pia Ngole alitoa wito kwa wanasheria wote wanaohitimu katika Taasisi hiyo kuwa tayari kutoa huduma popote pale nchini Tanzania kwa kuwa Serikali imetumia fedha nyingi kuanzisha Taasisi hiyo ili iwanufaishe wananchi wote. Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mitihani, Ipyana Mwaikambo alisema taasisi hiyo imeshadahili wanafunzi zaidi ya 4000 toka kuanzishwa kwake mwaka 2008 hadi sasa.
Naye Mmoja wa wanafunzi wa Taasisi hiyo, Edwin Rweykaza amesema Taasisi hiyo inatoa msisitizo katika mafunzo ya vitendo na kuwajengea uwezo wa kutimiza majukumu yao mara baada ya kuhitimu. Kuhusu maadili Rweykaza alibainisha kuwa ni swala linalopewa kipaumbele kwa wanafunzi wote wanaojiunga na Taasisi hiyo.
Serikali imetimiza ndoto ya miaka mingi ya kujenga majengo ya kisasa ya Taasisi ya Mafunzo ya uanasheria kwa vitendo Tanzania inayotoa mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu wa shahada ya kwanza ya sheria wanaotarajia kufanya kazi kama mawakili kwa lengo la kuongeza stadi na ujuzi wa wanasheria hao katika kuwahudumia wananchi.