Serikali Yatenga Bilioni Moja Ujenzi wa Daraja la Kavuu, Pinda Achangia Milioni 25 Ununuzi wa Jenereta Wilayani Mlele

Coat of Arms of Tanzania

Na Mwandishi Maalumu, Mlele

SERIKALI imetenga kiasi cha sh. bilioni moja kwa ajili ya kazi za awali za ujenzi wa daraja la mto Kavuu linalounganisha kata za Mamba, Kasansa, Majimoto, na kijiji cha Inyonga yalipo makao makuu ya wilaya mpya ya Mlele.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda jana jioni (Jumatano, Desemba 19, 2012) wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Mamba kwenye uwanja wa mpira akiwa katika siku ya saba ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi.

Waziri Mkuu alisema Serikali ina nia ya kufungua mawasiliano kati ya bonde la Rukwa na mikoa ya kaskazini ambako kuna uhaba wa chakula. “Bonde hili linasifika kwa uzalishaji mkubwa wa nafaka kwa hiyo kujengwa kwa daraja hilo ni ukombozi mkubwa wa kufungua soko kwa mazao mnayozalisha huku,” alisema.

Alisema katika mwaka huu wa fedha, barabara ya kutoka Sitalike kupitia Kibaoni, Majimoto, Mamba hadi Kasansa yenye urefu wa kilomita 33.5 imetengewa sh. milioni 837/- na kwamba wakandarasi wawili wamekwishapatikana ili kuifanyia ukarabati barabara hiyo. Kuhusu barabara ya Majimoto hadi Inyonga yenye urefu wa kilometa 135, Waziri Mkuu alisema zimetengwa sh. milioni 943/- kwa ajili ya ujenzi wa madaraja katika barabara hiyo.

Alipoulizwa kuhusu kuwepo kwa fedha hizo, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Katavi, Mhandisi Isaack Kamwelwe alimthibitishia Waziri Mkuu kuwepo kwa fedha hizo.

“Fedha zimeshatengwa na leo nimepokea kibali cha kutangaza zabuni za ujenzi wa daraja hilo. Zabuni zitatangazwa kuanzia Januari 2013,” alisema.

Kutokuwepo kwa daraja la Kavuu kunawafanya wakazi waishia bonde la Rukwa (maeneo ya Majimoto na Mamba) kila wanapotaka kwenda Inyonga, walazimike kupitia Mpanda yaliko makao makuu ya wilaya yao ambako ni zaidi ya kilometa 350. Desemba 21, 2012 Waziri Mkuu atakwenda kata ya Usevya ambako atazindua mradi wa umemejua kwenye sekondari ya kata ya Usevya na kuhutubia wananchi.

Wakati huo huo; WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ameahidi kuchangia gharama za ununuzi wa jenereta kwa ajili ya kata ya Majimoto wilayani Mlele mkoani Katavi ili waweze kuwa na umeme wa uhakika.

Ametoa ahadi hiyo Desemba 19, 2012 wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Majimoto kwenye uwanja wa mpira akiwa katika siku ya saba ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi.

“Kuna wafanyabiashara wa hapa Majimoto ambao walikuja kuniona na wakasema wako tayari kuchangia ununuzi wa jenereta lenye uwezo wa kutoa kilovoti 60 za umeme kwa nyumba kama 300. Wao watoe milioni 25 wakiwa tayari na mimi nitatoa milioni 25… jaribuni mkae na kupanga namna ya kuchangia gharama.”

“Baada ya muda fulani mtakuta mmemaliza kuchangia, tuwarudishie wafanyabiashara hela yao ili hilo jenereta liwe la kijiji. Mkilipata, nitawasiliana na TANESCO ili watupatie nguzo za umeme,” alisema.

Akijibu hoja kuhusu viwanja, Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Katavi alisema upimaji wa viwanja ulifanyika miaka miwili iliyopita na vikapatikana viwanja 270 lakini hadi sasa havijagawiwa kwa wananchi. Aliwataka viongozi wa kata na wilaya wasimamie zoezi hilo.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaonya juu ya ujenzi wa nyumba za makazi na biashara kando ya barabara kuu. ” Ninawasihi sana mheshimu sheria za barabara…msijenge nyumba zenu ndani ya hifadhi ya barabara. Desemba 21, 2012 Waziri Mkuu atakwenda kata ya Usevya ambako atazindua mradi wa umemejua (solar power) kwenye sekondari ya kata ya Usevya na kuhutubia wananchi.