WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge Mhe. William V. Lukuvi (Mb) amesema katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 109/= kwa ajili ya kununua Tani laki mbili za mahindi ya Hifadhi ya Chakula kwa Mikoa ambayo inauhaba wa chakula hapa nchini.
Alisema hayo Septemba 19, 2013 alipokuwa akifanya majumuisho ya ziara yake Wilaya Mbozi Mkoani Mbeya alipotembelea Wakala wa Taifa wa Hifadhi Chakula ya Vwawa ya mkoani humo. Alieleza kuwa, kutokana na tathmini iliyofanyika mwezi Agosti mwaka huu, imeonesha Wilaya kumi na Tisa nchini zitakuwa na upungufu wa chakula hivyo tani hizo laki mbili za mahindi zitasambazwa katika mikoa ya Dar es Salaam ambayo zitasaidia kanda ya Mashariki na Pwani na Mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya Kanda ya Ziwa.
Vilevile, Waziri aliwasisitiza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuanza mapema taratibu za kusafirisha mahindi hayo kabla kipindi cha mvua kuanza, na kusisitiza kuzingatia viwango vya mahindi yenye usafi na ubora kwani mahindi haya yanunuliwa kwa ajili ya kulisha Wilaya zenye uhaba wa chakula nchini na sivinginevyo.
“Kwa kuzingatia kanuni za utayarishaji wa mahindi na viwango bora vya usafi itasaidia kuuza na kusafirisha mahindi haya nchi za nje kama Sudan na nchi nyingine,alisisitiza Waziri Lukuvi,”.
Pamoja na hayo, Waziri Lukuvi alizishauri Wilaya kuanzisha vituo vya ununuzi wa mazao ya Nafaka angalau katika kila Tarafa kuwe na kituo cha kununulia Mazao, alisema, “vituo hivyo vitasaidia kuwa na bei moja ya ununuzi wa mazao ya nafaka ambapo pia itapunguza ulanguzi wa mahindi na vilevile kumsaidia Mkulima kufaidika na uuzaji wa mahindi kwani mtu yeyote atakaye hitaji kuuza mazao lazima akauzie kwenye kituo husika ambacho pia kitasaidia uingizaji wa mapato nchini”.
Katika ziara hiyo Waziri Lukuvi aliweza kujionea maendeleo mbalimbali katika Mikoa hiyo ikiwa ni pamoja na kutembelea kiwanda cha Kampuni ya Tawaqal kilichopo Mkoani Rukwa, kinachozalisha na kusambaza maji aina ya Dew Drop pamoja na kiwanda kinachozalisha unga aina ya Energ Milling, Waziri alikisifu kiwanda hicho cha kisasa chenye uwezo mkubwa wa kuzalisha maji lita 6000 kwa saa na kupongeza jitihada za Uwekezaji wa ndani nchini.
*Imeandaliwa na Ofisa Habari, Ofisi ya Waziri Mkuu