SERIKALI YATAKIWA KUIMARISHA KILIMO CHA UMWAGILIAJI

Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Bilal akiangalia moja ya mashamba ya kilimo cha umwagiliaji.

Na Janeth Mushi, Thehabari Arusha

SERIKALI kwa kushirikiana na taasisi binafsi imetakiwa kuimarisha
kilimo cha umwagiliaji ikiwa ni pamoja na kutoa elimu juu ya umuhimu wa kilimo hicho, badala ya kutegemea kilimo cha msimu ambacho si cha uhakika sana.

Wakulima wengi nchini wamekuwa wakilima kwa kutegemea hali ya hewa (mvua) hali inayosababisha wakati mwingine kiwango cha uzalishaji kupungua.

Changamoto hiyo imetolewa jana mjini hapa na Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya MOCROPS, Richard Modest katika maonesho ya 18 ya wakulima na wafugaji, Nane nane Kanda ya Kaskazini yanayoendelea kwenye viwanja vya Themi, Njiro.

Aidha, Modest alisema kuwa elimu zaidi inahitajika kwa wakulima ili kuweza kuondokana na kilimo cha mazoea ambacho kimekuwa hakina tija, na badala yake kuendesha kilimo chenye tija.

“Serikali iweke nguvu katika kilimo cha umwagiliaji kwa kutoa elimu kwa wakulima ili wakulima waweze kubadili mfumo wa kulima kwa mazoea na badala yake walime kilimo cha tija ambacho kitawaongezea uzalishaji na kipato kwani wakulima wengi wanategemea kilimo cha msimu ambacho hutegemea mvua.”

“Katika mikoa ya Kilimanjaro, Mwanza, Arusha, Mbeya kilimo cha
umwagiliaji kinakua kwa kasi kwa wakulima wa mbogamboga ambao tayari tumeshawapatia mafunzo ya umuhimu wa kilimo cha umwagiliaji na siyo kilimo cha kutegemea hali ya hewa ambayo kwa sasa imekuwa ikibadilika kila wakati,” alisema Modest.

Aidha Kampuni hiyo inayojihusisha na uuzaji wa pembejeo, mbegu na dawa za kilimo inatarajia kufungua mashine kwa ajili ya kubangua zao la Korosho ili kuwawezesha wakulima wa zao hilo kuweza kuuza bidhaa zao zikiwa tayari zimeshafungwa.

Alisema kuwa mashine hiyo inayotarajiwa katika wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara huku lengo la kampuni hiyo likiwa ni kumkomboa mkulima hapa nchini na kumuondoa katika kilimo kisicho cha tija.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa kwa kipindi cha mwaka huu wametumia
milioni 240 kwa ajili ya mafunzo kwa wakulima wa zao la Korosho katika maeneo ambayo zao hilo hupandwa huku milioni 80 zikiwa zimetumika mwaka jana kwa mafunzo kwa wakulima wa zao la Pamba.

“Elimu ya kilimo kwa wakulima ni changamoto kubwa kwani wakulima wengi hawana elimu juu ya kilimo cha kisasa hivyo elimu tunayoendelea kutoa kwa wakulima inawasaidia kuongeza ubora wa bidhaa zao ambazo zimekuwa na soko kubwa kimataifa,” aliongeza

Modest alisema kuwa wantarajia kuwafikia wakulima zaidi ya 25,000 na katika kumkomboa mkulima wanatarajia kufungua kiwanda mwaka huu
ambacho kitakuwa kinazalisha mbegu pamoja na bidhaa nyingine
zitakazoweza kumfikia mkulima kwa karibu.

Aidha aliomba Serikali kuhakikisha kuwa suala la malipo ya pembejeo yanafika kwa wakati kwani malipo yamekuwa yakichelewa hali inayosababisha kuchukua mikopo katika benki ya taasisi nyingine za fedha ambazo zinakuwa na riba kubwa.