Serikali Yasitisha Vibali vya Matangazo Tiba Asili

Matangazo dawa za asili

Matangazo dawa za asili


SERIKALI imesitisha vibali vya kurusha matangazo ya tiba za asili na mbadala kwenye vyombo vyote vya habari baada ya kubaini kuwa yanapotosha jamii.

Taarifa iliyotolewa na Baraza la Tiba za Asili na Tiba Mbadala kwa vyombo vya habari jana, inaeleza kuwa katika siku za karibuni kumekuwapo na matangazo mbalimbali ya tiba hizo ambayo baadhi yake hayaisaidii jamii. Kutokana na taarifa hiyo ya baraza, vyombo vya habari havipaswi kupokea kibali chochote cha kutangaza matangazo ya tiba hizo hivi sasa, kwa kuwa ni batili.

“Hivyo basi kituo chochote cha redio, luninga, mitandao na magazeti hayaruhusiwi kurusha tangazo lolote linalohusiana na mambo ya tiba asili na mbadala kwa kipindi hiki,” ilisema taarifa iliyosainiwa na Lucy Mziray.

Pia taarifa hiyo inaeleza kuwa, chombo chochote kitakachorusha tangazo au kipindi kitatozwa faini na kuchukuliwa hatua kali za kisheria. Akizungumzia uamuzi wa Serikali uliochukuliwa, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Primus Saidia alisema kuwa matangazo ya tiba mbadala na asili kwa muda mrefu yamekuwa yakipotosha umma kwa kukiuka Sheria ya Waganga na Tiba Mbadala ya mwaka 2002 inayowazuia kujiita madaktari na kujitangaza kwenye vyombo vya habari.

“Wanakwenda kinyume wanajiita madaktari, wengine maprofesa, halafu wanakwenda mbali zaidi na kuvaa vifaa vya udaktari kwenye televisheni ili kuwavutia watu,” alisema Dk Saidia.

Aliongeza: “Kuna watu wanatangaza kuwa wanatibu figo kwa siku saba jambo ambalo haliwezekani duniani kote, wanachofanya ni kuwachelewesha wagonjwa kwenda hospitali mapema.”

Naye mtaalamu wa tiba za asili, John Kidua, alisema serikali imefanya kosa kuyazuia matangazo yote badala ya kuwaadhibu watu waliobainika kuipotosha jamii pekee yao. Alisema upo uthibitisho kuwa baadhi ya dawa za asili zinatibu vizuri kuliko dawa za hospitali jambo ambalo limekuwa kikiokoa fedha nyingi za kuwasafirisha wagonjwa nje ya nchi.

“Ilitakiwa serikali itoe msaada kwetu ili tuongeze nguvu pale tunaposhindwa na siyo kutujumuisha wote kwenye kikapu kimoja,” alisema Kidua.
CHANZO: Mwananchi