SERIKALI imesitisha utaratibu wa kuvibadili Vyuo vya Ufundi kuwa Vyuo Vikuu ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa mafundi sanifu na uhaba wa vyuo vinavyotoa mafunzo ya ufundi sanifu katika nyanja ya uhandisi na teknolojia.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Januari 21, 2012 wakati akiwahutubia washiriki wa mahafali ya tatu ya Chuo cha Ufundi Arusha yaliyofanyika kwenye viwanja vya chuo hicho mjini Arusha.
Waziri Mkuu alisema Serikali imefanya hivyo kwa kutambua kuwa yapo mahitaji makubwa katika soko la ajira kwa wataalam wanaohitimu kutoka katika vyuo hivyo.
“Ili kukabiliana na changamoto hiyo, tumeamua kuchukua hatua hiyo ili kuimarisha elimu na stadi mbalimbali za ufundi, sayansi na teknolojia ili kukidhi mahitaji ya mafundi sanifu katika kutoa huduma za ufundi na uhandisi,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema Serikali imeamua kuruhusu Vyuo vya Ufundi vitoe tuzo endelevu hadi ngazi ya Shahada bila kuwa Vyuo Vikuu na bila kubadili madhumuni ya uasisi wake (Purpose of Establishment) ili mradi vifuate taratibu za Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).
Waziri Mkuu alisema ipo mifano mingi ya vyuo vya aina hiyo Duniani ambavyo vimekuwa na manufaa sana kwa jamii na vimesaidia kuongeza idadi ya mafundi sanifu na kukuza elimu ya ufundi na teknolojia.
Alivitaja baadhi ya vyuo hivyo kuwa ni: Taasisi ya Teknolojia ya Massachuset ya Marekani (Massachuset Institute of Technology); Taasisi ya Teknolojia ya Korea ya Kusini (Korea Institute of Technology); Chuo cha Ufundi cha Koforidua cha Ghana (Koforidua Polytechnic); na Taasisi za Teknolojia za India (Indian Institutes of Technology).
Alisema ili kuimarisha elimu na mafunzo ya ufundi nchini, Serikali kupitia NACTE iliamua kusajili vyuo vyote vya ufundi na kwamba hadi kufikia Juni 2011, jumla ya vyuo 240 vilikuwa vimesajiliwa.
“Hata hivyo, kati ya vyuo hivyo 240, vyuo vinavyotoa elimu na mafunzo ya ufundi katika nyanja ya uhandisi na teknolojia ni vyuo 39, sawa na asilimia 16 tu. Kati ya vyuo hivyo 39, vyuo vya Serikali havizidi sita ambavyo ni vichache sana kulingana na mahitaji yetu. Serikali itaweka mkazo mkubwa katika eneo hili kwa kuzingatia Mpango wa Maendeleo wa miaka 15,” alisisitiza.
Alitoa changamoto kwa uongozi wa chuo hicho kuangalia uwezekano wa kuanzisha mafunzo katika nyanja za utafiti, uchimbaji, usafishaji na usafirishaji mafuta, gesi na madini ya uranium, chuma na makaa ya mawe ili wahitimu hao waweze kuchukua nafasi za ajira zinazojitokeza.
Aliiomba Taasisi ya Elimu nchini (TEA) iangalie uwezekano wa kusaidia ujenzi wa bweni la wasichana ili kuongeza udahili wa wanafunzi wa kike katika chuo hicho. “Jumla ya wanafunzi wanaohitimu ni 231 na wote wanahitimu katika Stashahada ya Uhandisi. Kati yao, Wahitimu Wasichana ni 16 sawa na asilimia 7 tu.”
“Hali hii haiendani na maelekezo ya Ibara ya 85(f)(v) ya Ilani ya Chama Tawala ya mwaka 2010 hadi 2015 inayoelekeza:- Kuendelea kuhamasisha wanafunzi wa kike kujiunga na Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi.”
Aidha, Waziri Mkuu alisema idadi hiyo ndogo haiendani na dhamira ya Serikali ya kuwawezesha wanawake. “Upo umuhimu wa kuongeza idadi ya wasichana katika kozi zinazotolewa hapa chuoni,” alisisitiza.