*Yakana kupokea tamko la madaktari
Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Afya, Lucy Nkya amesema tamko lililotolewa na Chama cha Madaktari Tanzania la kutoa saa 72 kwa Serikali kuwarejesha madaktari walio katika mafunzo ya vitendo hospitali ya Taifa ya Muhimbili, pamoja na madai ya kuhamishwa vituo vya kazi halijawasilishwa rasmi wizarani.
Naibu huyo alifafanua kuwa madaktari hao hawajafukuzwa kufanya mazoezi bali kilichofanyika ni kuwarudisha wizarani na kuwapangia vituo vipya kutokana na uwezo mdogo wa hospitali hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana alisema baada ya wataalamu hao kugoma wizara ililazimikia kukabiliana na madhara yaliyotokana na mgomo huo kwa kuwapeleka wataalam wengine 51 kwa lengo la kuokoa maisha ya wananchi waliokuwa wakihitaji huduma za afya.
Nkya alisema wataalamu hao wanapaswa kuwa wazalendo kwa kurudisha fadhila kwa kuwatumikia wananchi kwa uaminifu kwani wamekuwa wakisomeshwa kwa kodi pia kuzingatia kiapo cha kutetea uhai kama walivyoapa.
“Nawakumbusha madaktari wenzangu kuwa tunapokula kiapo tusikiuke kwani ni kumdhihaki mwenyezi Mungu mgomo ni ukiukwaji wa kiapo kwani hatuwezi kutetea uhai tukiwa tumegoma,” alisema.
Alisema wataalamu wote wa sekta ya afya wanasimamiwa na mabaraza maalum ambayo ni mamlaka zilizoanzishwa kwa sheria za bunge na kupewa dhamana ya kusimamia utendaji na uendelezaji taaluma zao kwa kuzingatia maadili na miiko iliyoainishwa na taaluma husika.
Alibainisha kuwa serikali kwa kuthamini taaluma za sekta ya afya imeweka msukumo katika kuendeleza wataalamu wake kielimu kwa kuongeza idadi ya vyuo, wanafunzi wanaofanyiwa udahili pia kugharimia mafunzo yao ya shahada ambapo kila mwanafunzi anagharimiwa kati ya milioni 2 mpaka 3.7 kwa mwaka kwa muda wa miaka 3 mpaka 5 pamoja na kupata uhakika wa ajira baada ya kumaliza mafunzo.
Wataalamu hao wamegawanywa katika hospitali za Muhimbili ambapo madaktari ni 86, wafamasia 35 na wataalamu wa maabara 13, Hospitali ya rufaa Temeke jumla ya wataalamu 12, Amana 19, Mwanayamala 16, hospitali ya Jeshi ya Lugalo 7 na Hospitali ya Aga Khan 7.
Aidha alisema ni madaktari 10 walioripoti na kuendelea na kazi ya kuhudumia watanzania katika hosipitali za rufaa kati ya 61 waliopangwa mwaka jana katika hospitali hizo za rufaa mkoa na manispaa za Jjiji la Dar es Salaam.
“Wizara inawapongeza wale waliotekeleza agizo la uhamisho na inatarajia kuwa waliobaki wataripoti katika vituo vyao vya kazi ili jamii ya maeneo hayo iweze kupata huduma za ubingwa wanazostahili,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa sheria na kanuni za utumishi wa umma suala la kituo cha kazi linategemea na malengo yaliyowekwa na nchi kulingana na mahitaji katika sehemu mbalimbali nchini hivyo uhamisho wa madaktari hao wenye shahada ya uzamili wa fani mbalimbali ulifanyika kwa kuzingatia dhana hiyo.