Serikali Yasalimu Amri, Yakubali Madai ya Madereva

Kamanda wa kikaosi cha Usalama Barabarani Ndugu Mohamedi Mpinga.

Kamanda wa kikaosi cha Usalama Barabarani Ndugu Mohamedi Mpinga.


Na Pius Yalula, Maelezo – Dar es Salaam

SERIKALI imesema hakutakuwa na mafunzo kwa madereva wa malori na mabasi na wala hawatakiwi kwenda kusoma kozi fupi ili kuhuisha leseni zao kama ilivyokuwa imetangazwa hapo awali na kusababisha mgomo.
Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mohamed Mpinga wakati akitoa tamko hilo kwa waandishi wa habari leo mjini Dar es salaam.

Alisema kuwa madereva wenye daraja E, C, C1, C2 na C3 walitakiwa kupata mafunzo ya muda mfupi kila baada ya miaka 3 kulingana na kanuni ziliandaliwa mwaka 2014 kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), Chuo cha Taifa ya Usafishaji (NIT), Vyama vya Madereva, Ofisi ya Mwanasheri Mkuu wa Serikali na Chama cha Wamiliki wa Magari ya Mizigo Tanzania (TATOA), lakini kwa mwaka huu hawatatekeleza kanuni hiyo.

Kamanda Mpinga alisisitiza kuwa kanuni hiyo haitatumika mwaka huu badala yake madereva wataendelea na utaratibu wao wa zamani wa kubadilisha na kuhuisha leseni zao kwa zile ambazo zitakuwa zimekwisha bila kuulizwa vyeti.
Aliongeza kuwa hadi hivi sasa mitala ya mafunzo hayo ya muda mfupi bado haijakamilika na wala Serikali haijawahi kupanga ada za mafunzo hayo, kwa hiyo utaratibu wa zamani utaendelea kutumika kama ulivyokuwa hapo awali.
Kamanda Mpinga alitoa wito kwa madereva wote kuwa wavumilivu kwa matatizo yao wakati Kamati ya kudumu ya kutatua matatizo ya sekta ya usafishaji ikendelea kuyatafutia ufumbuzi.

Katika hatua nyingine Kamanda huyo ametoa wito kwa wananchi na wasafiri kutoa taarifa kwa viongozi wa jeshi hilo endapo wanaona askari wao au dereva anatenda vitendo visivyo vya kimaadili ili aweze kuchukuliwa hatua.
Alisema kuwa jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani kipo wakati tayari kupokea malalamiko ya kuyachukulia hatua ili kulinda maisha ya wasafiri na mali zao , hivyo ni vizuri wakaripoti wale wote wanaohatarisha maisha ya wenzao.