Frank Mvungi, Maelezo
SERIKALI imetoa usajili kwa makampuni 51 ya wakala Binafsi wa Huduma za ajira nchini kati ya 87 yaliyowasilisha maombi yake kwa Kamishna wa kazi. Taarifa hiyo imetolewa Jijini Dar es Salaam na Msemaji wa Wizara ya Kazi na Ajira, Ridhiwan Wema wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Alisema makampuni yaliyosalia 36 hayakupata usajili kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutokidhi vigezo na kukosa nyaraka muhimu. Akitaja baadhi ya makampuni yaliyopewa usajili baada ya kukidhi vigezo kuwa ni PA Ppospect Africa, Delloitte, KPMG Advisory Ltd, People Ltd, HR-Solutions na AGP Consultants.
Akifafanua zaidi Wema alisema kuwa kampuni au wakala yoyote ambaye hajapata usajili hatoruhusiwa kufanya kazi ya uwakala binafsi wa huduma za ajira hapa nchini. Katika Kushughulikia suala la usajili Wema amesema kuwa Wizara imeandaa kanuni chini ya sheria ya ukuzaji wa huduma za ajira Na.9 ya mwaka 1999 na kutangazwa kupitia tangazo la Serikali Na. 232 la tarehe 11 Julai 2014.
Aidha Wema alitoa wito kwa makampuni au mtu yeyote anayetaka kufanya shughuli za huduma za ajira kuzingatia taratibu na kanuni chini ya Sheria ya kukuza huduma za ajira Na. 9 ya Mwaka 1999.
Aliongeza kwamba ukodishaji wa huduma (outsourcing of Services) haujapigwa marufuku bali kilichopigwa marufuku ni ukodishwaji wa watu (outsourcing of persons) hivyo ni marufuku kwa wakala wa huduma za ajira kuajiri na kukodisha wafanyakazi au kuajiri kwa niaba ya kampuni nyingine na wakala hao kuwa sehemu ya mahusiano ya ajira yanayoweza kujitokeza baina ya watafuta kazi na waajiri.
Januari 27, 2014, Waziri wa Kazi na Ajira, Bi. Gaudensia Kabaka alitoa tamko la Serikali kuhusu uendeshaji wa wakala binafsi wa huduma za ajira nchini, hii inatokana na Wizara hiyo kupokea malalamiko toka kwa wadau mbalimbali kuhusu utaratibu wa udalali wa kukodisha wafanyakazi katika makampuni unaofanywa na baadhi ya wakala binafsi wa huduma za ajira nchini.