SERIKALI ya Tanzania na Uganda zimesaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano (BASA), katika usafiri wa anga utakaowezesha nchi hizo kutoa huduma bora za anga na kufungua fursa za kibiashara kwa wananchi wake.
Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo jijini Arusha, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema mkataba huo utaruhusu ndege za nchi hizo mbili kutua na kuruka bila vikwazo vyovyote katika nchi hizo.
“Naamini ushirikiano huu utaboresha huduma zinazotolewa na Mamlaka za usafiri wa Anga na hivyo kuongeza viwango vya usalama wa usafiri huu”, amasesema Prof. Mbarawa.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Sam Kutesa, amesisitiza kuwa mkataba huo ni muendelezo wa ushirikiano mwema baina ya Tanzania na Uganda na hivyo kuchochea maendeleo ya uchumi kwa raia wa nchi hizo.
Ushirikiano wa Tanzania na Uganda ni sehemu ya mkakati wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kuwezesha wananchi wake kunufaika na fursa za kijamii, kiuchumi, kiusalama na kiutamaduni.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.