Serikali Yapongeza Operesheni Safisha ya TFDA

Dk. Hamisi Kigwangala

NAIBU WAZIRI WA AFYA, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla amepongeza juhudi za Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) nchini kwa hatua wanazochukua katika utendaji wake ikiwemo zoezi la kukagua madawa yasiyofaa kwa Jamii ikiwemo yale yaliyokwisha muda wake hasa katika zoezi la “Operesheni Safisha” iliyofanywa karibu mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara huku akitaka wale wote waliohusika kupandishwa Mahakamani kwa hatua za kushughulikiwa.

Kigwangalla ameyasema hayo mapema jana Machi 17 jijini Dar es Salaam baada ya kupewa matokeo ya Operesheni Safisha kwa maduka ya dawa muhimu na yasiokuwa na vibali iliyofanywa na Baraza la Wafamasia na TFDA pamoja na Jeshi la Polisi, amesema dawa zilizokamatwa zitaifishwe na kupeleka katika hospitali za serikali.

Amesema kuwa haiwezekani wananchi wakakosa dawa za serikali na kuonekana katika maduka ya dawa na watu hao wakaachwa bila kuchukuliwa hatua. Kigwangalla amesema kuwa katika operesheni hiyo baadhi ya maduka yanauza dawa ambazo haziko kwenye orodha za dawa ikiwemo ni dawa ya usingizi ambayo inatakiwa kutumika wakati wa operesheni.

Aidha amesema kuwa baadhi ya maduka mengine yamefungwa lakini yanauza dawa nyakati za usiku na kuwataka wanaofanya operesheni kuendelea na wataokutwa wachukuliwe hatua mara moja.

Operesheni hiyo ilianza machi 1 hadi 3 mwaka huu ambapo walikagua maduka 685 katika mikoa tisa na kati hayo maduka 432 yamefungiwa kwa sababu mbalimbali ikiwemo na kuwa na dawa za serikali pamoja na kuwa dawa za asili.

Aidha amesema dawa ni sumu hivyo inatakiwa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na wanaouza dawa ambazo hawana orodha nazo wanazalisha matatizo ya kiafya kwa wananchi
Kigwangalla amesema hadi sasa ni dawa 65 tu ndiyo zenye nembo ya serikali na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano pale watakapopata dawa serikali katika duka la dawa. Amesema kuwa jeshi la polisi lichukue hatua ya kuwabana wale wote waliokutwa na dawa za serikali kuwabana katika kuweza kuwapata waliokuwa wakiwapa dawa hizo.