WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amezipiga marufuku timu za Simba na Yanga kutumia uwanja wa taifa kwa michezo yake yoyote zinapokuwa zikicheza. Waziri Nape ametoa katazo hilo baada ya mashabiki wa clabu za timu hizo kuvunja viti pamoja na mageti ya kuingilia jana katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambapo Simba na Yanga walipambana na timu zote kutoka sare ya bao moja kwa moja (1-1).
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu washabiki wa Simba walivunja viti vya uwanja wa taifa baada ya kufungwa goli na Yanga kwa madai goli lililofungwa halikuwa halali hivyo muamuzi aliibeba Yanga. Baada ya kuingia kwa bao hilo ambalo mashabiki wa Simba walionekana wakilalamika kuwa mfungaji alifunga kwa mkono walipandwa na ghadhabu na kuamua kung’oa viti walivyokalia na kuanza kurusha uwanjani jambo lililosababisha kusimama kwa mpambano huo kwa dakika kadhaa.
Waziri Nape alisema mashabiki wa pande zote hawakuonekana wastarabu kwa kuwa kabla ya tukio hilo mashabiki wa Yanga na Simba pia walivunja mageti ya kuingilia uwanjani jambo ambalo si la kiungwana hivyo wameamua kusimamisha timu hizo kutumia uwanja wa taifa kwa muda usiojulikana.
Alisema Serikali pia imezuia mapato ya mchezo huo ili kufanya tasmini ya hasara waliyoifanya katika mchezo huo na clabu zote zitalazimika kulipa kwanza kabla ya kupata mapato yao. Alisema kwa sasa si Yanga wala Simba zitaruhusiwa kutumia uwanja huo bila kujali wanacheza wao ama timu zingine dhidi yao hadi hapo Serikali itakapo toa taarifa nyingine. Hii si mara ya kwanza mashabiki wa timu hizo kufanya hasara katika uwanja huo huku zikiadhibiwa clabu jambo ambalo mashabiki wamekuwa hawaumii na adhabu hizo.