Serikali yapeleka madaktari wa Jeshi Muhimbili

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI ya Tanzania imelazimika kuchukua madaktari 15 kutoka Hospitali ya Jeshi la Wananchi Tanzania ya Lugalo na kuwapeleka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ya jijini Dar es Salaam ili kuziba pengo la madaktari waliogoma kutokana na madai anuai.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda amesema huduma za matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili zimeanza kurejea katika hali yake ya kawaida baada ya madaktari 15 kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kuanza kutoa huduma katika hospitali hiyo.

Amesema baada ya madaktari hao kuanza kufanya kazi hali kwa sasa katika jiji la Dar es Salaam ni ya kuridhisha ambapo katika Hospitali ya Muhimbili baadhi ya vitengo madaktari wa JWTZ wameziba mapengo. Madaktari hao wamepelekwa kutoa huduma kutokana na mgomo wa madaktari unaoendela katika maeneo mbalimbali nchini.

Mgomo wa madaktari hapa nchini ulianza Januari 16 mwaka huu ambapo madaktari wanaidai Serikali madai yao mbalimbali ikiwemo nyongeza ya mishahara, fedha za kufanyakazi wakati wa usiku na katika mazingira hatarishi pamoja na kupandishwa vyeo kwa wakati.

Kufuatia mgomo huo juzi Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitoa agizo akiwataka madaktari hao kurejea kazini mara vinginevyo ajira zao zitakoma, hata hivyo baadhi ya madaktari wamepuuza agizo hilo la Waziri Mkuu hali iliyoilazimu Serikali kuwachukuwa madaktari kutoka JWTZ kwa ajili ya kutoa huduma katika hospitali.