Serikali Yaongeza Muda Sensa ya viwanda Nchini

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar Es salaam kueleza uamuzi wa Serikali kuongeza muda wa Sensa ya Viwanda Tanzania Bara hadi Agosti 31,2015 na hatua zitakazochukuliwa kufuatia viwanda 366 kushindwa kuwasilisha takwimu za uzalishaji kwenye Madodoso ya Sensa.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar Es salaam kueleza uamuzi wa Serikali kuongeza muda wa Sensa ya Viwanda Tanzania Bara hadi Agosti 31,2015 na hatua zitakazochukuliwa kufuatia viwanda 366 kushindwa kuwasilisha takwimu za uzalishaji kwenye Madodoso ya Sensa.

Kaimu Meneja wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Mkoa wa Dar es salaam Bw. Albert Kapala akitoa ufafanuzi wa lengo la Sensa ya Viwanda na Idadi ya viwanda vilivyotoa taarifa za Sensa hiyo jijini Dar es salaam. Picha Na Aron Msigwa-MAELEZO

Kaimu Meneja wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Mkoa wa Dar es salaam Bw. Albert Kapala akitoa ufafanuzi wa lengo la Sensa ya Viwanda na Idadi ya viwanda vilivyotoa taarifa za Sensa hiyo jijini Dar es salaam. Picha Na Aron Msigwa-MAELEZO


Na Aron Msigwa-MAELEZO

SERIKALI imeongeza muda wa mwisho wa kukamilisha zoezi la ukusanyaji wa takwimu za Sensa ya viwanda kote nchini hadi Agosti 31, 2015 kufuatia viwanda vipatavyo 366 vilivyoko jijini Dar es salaam kushindwa kuwasilisha taarifa muhimu za uzalishaji kwenye madodoso ya Sensa hiyo.

Akitoa taarifa hiyo ya kuongezwa muda wa Sensa leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Saidi Meck Sadiki amesema kuwa Viwanda 366 ambayo ni sawa na asilimia 20 katika jijini Dar es salaam vimeshindwa kukamilisha na kurudisha madodoso ya taarifa muhimu za viwanda hivyo.

Alisema Sensa hiyo ilianza Machi 9 mwaka huu na ilitarajiwa kukamilika Juni 8, 2015 lengo likiwa kukusanya takwimu sahihi zinazohusu Sekta ya Viwanda na mchango wake katika uchumi wa Tanzania. Alisema Sensa hiyo pamoja na mambo mengine ililenga kupata viashiria sahihi vya uchumi pamoja na taarifa muhimu za viwanda zikiwemo orodha ya viwanda kimkoa, anuani na mahali vilipo, aina ya umiliki na utaifa wa wamiliki.

Takwimu nyingine ni mwaka ambao viwanda hivyo vilianza uzalishaji, shughuli kuu ya viwanda husika, idadi ya wafanyakazi waliopo, gharama za malipo mbalimbali kwa wafanyakazi, mapato yanayotokana na uzalishaj na gharama za uzalishaji.

Alibainisha kuwa mwaka 2013 Serikali iliamua kuwa ifanyike Sensa ya viwanda nchi nzima ili kubaini viashiria vya uchumi vitakavyosaidia kuweka mabadiliko ya muundo wa sekta ya viwanda na mchango wake katika pato la Taifa, kuboresha Sera na Programu za kukuza ajira, utekelezaji wa Malengo ya Milenia, Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025, MKUKUTA na Mpango wa Taifa wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).

Aidha, ameeleza kuwa jijini Dar es salaam kazi nzuri imefanyika kwa wenye viwanda kutoa ushirikiano kwa kukamilisha ujazaji wa madodoso mafupi na marefu na tayari madodoso hayo yameshawasilishwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa uchambuzi.

Saidi Meck Sadiki amefafanua kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara inaendelea kuhakikisha kuwa asilimia 8 iliyobaki ya viwanda vyote nchini inawasilisha taarifa husika kabla ya muda uliopangwa. Alisisitiza kuwa zoezi hilo liko kwa mujibu wa sheria ya takwimu ya mwaka 2012 na watakaoshindwa kutekeleza ujazaji wa madodoso hayo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

“Zoezi hili ni muhimu sana kwa ukuaji wa uchumi wa taifa letu linatupa picha ya sekta ya viwanda nchini pamoja na kuongeza uwazi katika mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa, hili lazima tulisimamie, wenye viwanda lazima watii sheria,” alisema.

Kwa upande wake Kaimu Meneja Takwimu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mkoa wa Dar es salaam, Albert Kapala amesema kuwa Zoezi hilo ni la kitaifa hivyo taarifa zote zinazokusanywa ni siri na zinatumika kwa matumizi ya kitakwimu tu. Alisema katika Sensa hiyo iliyoanza mwezi Machi mwaka huu mkoa wa Dar es salaam ulitarajia kuwa umekusanya takwimu za viwanda 1840 ifikapo Juni 8 mwaka huu.

Aliongeza kuwa hadi sasa viwanda vilivyoshindwa kuwasilisha taarifa kwa mujibu wa Sensa hiyo jijini Dar es salaam ni 366 wakati vilivyowasilisha ni 1474.