Na Mwandishi Wetu, Rombo
SERIKALI imeombwa kudhibiti utengenezaji holela wa pombe za kienyeji katika Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro ambao umekuwa hauzingatii afya ya mtumiaji. Baadhi ya viongozi wilayani hapa wameshauri pombe hizo sasa kuangaliwa ili zitengenezwe kwa kuzingatia viwango vinavyo faa kwa afya ya watumiaji na kuiwezesha serikali kupata mapato.
Ombi hilo limetolewa na madiwani wa halmashauri hiyo walipokuwa kwenye mdahalo wa uwajibikaji wa wabunge na madiwani ulioandaliwa na asasi ya Mfuko wa Elimu Rombo kwa udhamini wa Shirika la ‘Foundation for Civil Society’ huku lengo likiwa ni kutambua uwajibikaji wa viongozi katika kuitumikia jamii na utekelezaji wa sera kwa ujumla.
Utengenezaji wa pombe hizo ambazo umeathiri nguvu kazi ya taifa hususani vijana kwa sasa imezidi kushamiri, ambapo kuna pombe za kienyeji zaidi ya 40 zinazotengenezwa eneo hili na hazizingatii viwango kwa afya ya watumiaji.
Wakizungumza kwa wanyakati tofauti baadhi ya madiwani hao walisema pombe zinazotengenezwa wilayani Rombo hazina viwango vya kulinda afya ya mtumiaji na kwa sasa vijana wengi wamejiingiza kwenye ulevi ambao unachangia vijana hao kujiingiza kwenye vitendo viovu ikiwemo utumiaji wa dawa za kulevya pamoja na wizi.
Mratibu wa mdahalo huo, Inocent Malamsha ameiomba serikali kuchukua hatua za dhati katika kudhibiti watoto ambao wanaacha masomo na kukimbilia kufanya biashara katika masoko ya laitokitoki , last , Rombo kibung’a na Ndarara yaliyopo nchini Kenya.
Akifungua mdahalo huo kwaniaba ya Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Elinas Palanjo, Ofisa Tarafa ya Tarakea, Steven Nyela, pamoja na kuipongeza asasi hiyo, amewataka wabunge na madiwani kushirikiana na asasi mbalimbali, kuwasaidia wananchi kutekeleza miradi ya maendeleo, iliwaondokane na umaskini .