Pretoria, Afrika Kusini
RAIS wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema Serikali yake haikusudii kujenga barabara ya lami kukatisha mbuga maarufu duniani ya Serengeti iliyoko Kaskazini Mashariki mwa Tanzania.
Rais Kikwete amesema kuwa kama yupo kiongozi ambaye amethibitisha wakati wote wa uongozi wake kuwa mtetezi mkubwa wa mazingira na kulinda mbuga za wanyama basi ni yeye mwenyewe.
“Serengeti ni tunu ya taifa letu. Kamwe hatuwezi kuchukua hatua zozote za kuharibu ama hata kuvuruga hali ya Serengeti. Ni tunu ya Tanzania, ina thamani kiuchumi kwa wananchi wetu na kwa nchi yetu na ni moja ya maeneo machache duniani ambayo dunia inayatambua kwa upekee na umuhimu wake na inayalinda,” amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema hayo juzi, Jumanne, Julai 19, 2011 wakati anamjulisha Rais wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Jacob Zuma na mawaziri wa Baraza la Mawaziri la kiongozi huyo wa Afrika Kusini kuhusu mkanganyiko ambao umezuka, kwa bahati mbaya sana duniani, kuhusu mipango ya Serikali ya Rais Kikwete kuwapatia wananchi wanaoishi Kaskazini mwa Mbuga ya Serengenti barabara ya uhakika ili kumaliza matatizo yao makubwa ya maendeleo.
Rais Kikwete alitoa maelezo hayo kwa viongozi hao wa Afrika Kusini wakati wa mazungumzo rasmi kati ya Serikali za Tanzania na Afrika Kusini kwenye Majengo ya Muungano (Union Buildings) mjini Pretoria, Afrika Kusini.
Mazungumzo hayo yalikuwa moja ya shughuli za mwanzo kati ya shughuli nyingi za Mheshimiwa Rais Kikwete wakati wa ziara yake ya kidola ya kihistoria ya siku tatu katika Afrika Kusini iliyomalizika jioni ya leo, Jumatano, Julai 20, 2011. Rais Kikwete anaondoka Afrika Kusini kurejea nyumbani kesho, Alhamisi, Julai 21, 2011.
Rais Kikwete alimwambia Rais Zuma na mawaziri wake kuwa umekuwepo mchanganyiko usiokuwa wa lazima kabisa kuhusu mipango ya Serikali kuwapatia barabara wananchi wa maeneo yasiyofikika kwa urahisi kati ya Mto wa Mbu, mkoani Arusha hadi Makutano, mkoani Mara kupitia Loliondo, Mugumu na Nata.
“Nataka kuzungumzia kidogo suala la madai kuwa Tanzania inataka kujenga barabara ya lami kukatisha Mbuga ya Wanyama ya Serengeti. Sijui mkanganyiko kuhusu suala hili umetoka wapi lakini ukweli ni kwamba Serikali ya Tanzania haikusudii na wala haina mipango ya kujenga barabara ya lami kupitia mbuga hii muhimu sana kwa Tanzania na kwa dunia nzima.”
“Tunachosema ni kwamba Serikali yetu inao wajibu wa aina mbili. Kwanza ni kuhakikisha kuwa Watanzania wanaoishi Kaskazini mwa Serengeti wanapatiwa barabara ya uhakika ili kusaidia kufungua fursa zao za maendeleo.
Hawawezi kuendelea kufanywa kama sehemu ya utalii kwa kubakia katika hali ya udhalili. Pili ni kuhakikisha kuwa tunalinda Mbuga la Serengeti kama ambavyo tumefanya miaka yote tokea uhuru wetu mwaka 1961.”
“ Mipango yetu ni kuhakikisha kuwa sehemu nzima ya barabara inayokatisha Mbuga hiyo inabakia bila lami na wala siyo kweli kuwa tunalenga kuharibu Mbuga hiyo. Sisi ndio watunzaji wakuu wa mbuga hii na mbuga zote za wanyama za Tanzania, inakuwaje leo sisi ndiyo tunaambiwa kuwa tunakusudia kuharibu mbuga hizo? Binafsi tokea kuchukua nafasi ya Urais wa Tanzania mapumziko yangu yamekuwa katika mbuga zetu za wanyama…hata juzi, siku nne kabla ya kuja hapa nilikuwa Serengeti.”
Aliongeza Mheshimiwa Rais Kikwete: “Ni jambo la kusikitisha sana kuwa wapo watu ambao wanapinga ujenzi wa barabara hii ambayo wala haitakatisha kwa lami katikati ya mbuga hiyo. Wanasahau kuwa hawa watu tunaotaka kuwajengea barabara waliondolewa katika Mbuga hiyo ambamo walikuwa wanaishi. Waliondoka bila matatizo yoyote sasa kwa nini Serikali isiwajibike kwa kuwapatia nyenzo muhimu ya maendeleo kama barabara.”
Baada ya maelezo hayo, Rais Zuma alimwambia Rais Kikwete: “Tunaunga mkono moja kwa moja msimamo wa Tanzania kuhusu suala hili. Tunaelewa tatizo ambalo Serikali yako, Mheshimiwa Rais, inajaribu kulitatua la kuleta maendeleo kwa wananchi wake.”
Barabara ya Mto wa Mbu-Loliondo-Mugumu-Nata-Makutano yenye kilomita 452 ni miongoni mwa barabara zenye jumla ya kilomita 11,000 ambazo Serikali ya Rais Kikwete anazijenga ama kuanza kuzijenga katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake. Kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, ujenzi wa barabara hiyo unatakiwa kuanza katika kipindi cha sasa.
Akizungumza baadaye usiku katika dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na Rais Zuma kwa ajili yake kwenye Nyumba ya Urais ya Afrika Kusini, Rais Kikwete aliisifu Serikali ya Afrika Kusini kwa kuonyesha uongozi katika kukabiliana na changamoto zinazolikabili Bara la Afrika.
“Mheshimiwa Rais tulishughulikia kwa pamoja matatizo ya Burundi na sasa nchi hiyo imetulia. Umeshughulikia suala la Zimbabwe ambalo bado linahitaji jitihada zako. Kwa pamoja tulihangaika na Ivory Coast na tunawatakia heri waanze kuijenga upya nchi hiyo na sasa una changamoto ya Libya. Napenda kukupongeza kwa mchango wako katika kuleta utulivu na amani katika Bara letu.”