SERIKALI imetenga sh. bilioni 31 kwa ajili ya mradi wa Mbwinji wilayani Masasi utakaohudumia pia wilaya ya Nachingwea. Rais Jakaya Kikwete alisema hayo jana mjini Masasi katika uwanja wa sabasaba alipokuwa akihutubia wananchi.
Mradi huo mkubwa ambao chanzo chake cha maji ni Mto Nanguu unagharamiwa na serikali unatarajiwa kukamilika katikati ya mwaka 2012.
Rais yuko mkoani Mtwara kuwashukuru wananchi kwa kumchagua yeye na Chama chake Cha Mapinduzi kuliongoza tena Taifa la Tanzania na pia kukagua utekelezaji wa ahadi za uchaguzi.
Tatizo la maji ni kero kubwa kwa wananchi wa wilaya nyingi mkoani humu ikiwemo Masasi na Nanyumbu.
Mara baada ya kuwasili wilayani Masasi Rais amepokea taarifa ya wilaya za Masasi na Nanyumbu na kusikitishwa na taarifa za kuongezeka idadi ya watoto wanaopata mimba katika shule za msingi na sekondari
“Sijafurahishwa na mimba za watoto wa kike wa shule za msingi na sekondari si jambo jema”. Rais amesisitiza na kuwataka wanaume waache watoto wasome.
“Wanaume ndiyo chanzo cha tatizo hili, ni jambo la ovyo na watoto wa kike shughulikeni na jambo moja tu”. Rais amewaasa.
Rais ameshatembelea wilaya za Mtwara Mjini, Vijijini, Tandahimba, Newala, Masasi na Nanyumbu ambapo amemalizia ziara yake ya kikazi mkoani Mtwara na anatarajia kurejea jijini Dar es Salaam leo tarehe 29 Julai, 2011.