Na Anitha Jonas – MAELEZO
Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bw.Assah Mwambene ameutaka uongozi wa Gazeti la Dira ya Mtanzania kukanusha haraka na kuiomba radhi Serikali na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue kutokana na taarifa waliyoitoa katika toleo namba 404 la tarehe 29/02/2016 lenye kichwa cha habari “Uchafu wa Ombeni Sefue Ikulu.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi huyo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu taarifa kuwa hazikuwa na ukweli wowote kwani Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue hakuhusika katika uteuzi wa Mkurugenzi wa MSD wala kuhusika na kampuni ya CRJE katika utoaji wa tenda ya kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma Oktoba 2007 kwani katika kipindi hicho alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani.
“Serikali inautaka uongozi wa Gazeti la Dira ya Mtanzania ukanunushe taarifa hiyo kwa uzito ule uliyotumika kuchapisha habari hiyo na kama wanapinga wakidai wana ushahidi basi waupeleke mara moja kwenye vyombo vinavyohusika ikiwemo Sekretarieti ya Maadili na TAKUKURU”,alisema Bw.Mwambene.
Aidha, Bw.Mwambene amesema gazeti hilo liliandika kuwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue alipigia chapuo Kampuni ya “UGG” iliyowahi kuonyesha nia ya kujenga reli ya Kati nchini. Taaarifa hii pia siyo ya kweli na hakuna kampuni yenye jina la “UGG” ilishawahi kuonyesha nia ya kujenga reli hiyo.
Mkurugenzi aliendelea kusema kuwa gazeti hilo lilimtuhumu pia Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue kuhusika na kumsafisha Bwana Eliakim Maswi wakati alichokifanya Balozi Sefue ilikuwa ni kusoma matokeo ya uchunguzi ambao hakuufanya yeye. Waliomsafisha ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Kamati ya Uchunguzi iliyoongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu kwani ndio waliiyofanya uchunguzi huo.
Hata hivyo serikali imewashauri wamiliki wa vyombo vya habari,wachapishaji,wahariri, na waandishi wa habari wajikite kwenye weledi na ukweli pia wafanye utafiti wa kina na kuandika mambo waliyo na uhakika nayo.