Serikali Yakaza Uzi Matumizi ya EFD kwa Wafanyabiashara

Mgomo wa matumizi wa mashine za EFD kwa wafanyabiashara Kariakoo. (PICHA NA DJ SEK)

Mgomo wa matumizi wa mashine za EFD kwa wafanyabiashara Kariakoo. (PICHA NA DJ SEK)

SERIKALI imesema kuwa mgomo wa wafanyabiashara hauwezi kubadili uamuzi wake wa kukusanya kodi kupitia mashine za elektroniki za EFD na imewataka wafanyabiashara hao kufungua maduka yao kwa sababu hata wakiyafunga watatakiwa kuwa nazo.

Hatua hiyo ya Serikali imekuja ikiwa ni siku ya pili tangu wafanyabiashara hao walipogoma kufungua maduka wakipinga kutumia mfumo huo wa ulipaji kodi. Aidha, imeliagiza Jeshi la Polisi kusaka wafanyabiashara wanaotishia usalama wa mali za wenzao wakiwashinikiza kugoma kwa kisingizio cha kupinga matumizi ya mashine hizo.

Hata hivyo, Serikali imesikia kilio cha wafanyabiashara hao kuhusu bei ya mashine hizo na imetangaza kupunguza na sasa zitauzwa kati ya Sh600,000 hadi Sh778,000 badala ya Sh800,000 hadi 1.5milioni.

Wakizungumza kuhusu suala hilo kwa nyakati tofauti jana, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene waliwataka wafanyabiashara kuacha mgomo kwa kuwa ni kinyume cha sheria.
Waziri Mkuu alisema kuwa mashine hizo zilizotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iko sahihi kabisa na kuwa haiwezi kuacha kukusanya mapato kwa njia ya mashine hizo.

Akizindua miradi wa maji katika Shule ya Msingi Olomitu, Kata ya Mlangarini, Arusha, Pinda alisema mashine hizo hazina tatizo na kwamba TRA haina mpango wa kubadili msimamo wake wa kuzitumia. Mbali ya uamuzi wa kupunguza bei, Waziri Mkuu alisema wafanyabiashara wanapaswa kukumbuka kuwa gharama za ununuaji wa mashine hizo mwishowe zitabebwa na TRA kwani watarudishiwa fedha hizo kadri watakavyokuwa wanazitumia kwa mfumo wa makato.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mbene alisema: “Hawa waliogoma si kweli kwamba hawajapata elimu kuhusiana na utumiaji wa mashine hizo ila kuna waliopata elimu na kupata msukumo kutoka kwa wenzao na wengine walipata elimu hiyo lakini haikuwasaidia.”

“Mgomo huu umeleta usumbufu mkubwa siyo hapa nchini tu, bali hata katika nchi za Afrika Mashariki na Kati kwa wale wanaotegemea maduka hayo.”

Naibu wa waziri huyo alisema Serikali kupita TRA, ilianzisha mashine hizo kwa lengo la kuondoa usumbufu wa wafanyabiashara kukatwa kodi kubwa kwa kukisia, kumrahisishia mfanyabiashara kutunza kumbukumbu na kuondoa usumbufu wa kukisia kukata kodi.

Akizungumzia mgomo huo Mbene alisema: “Tumegawana majukumu. Sisi tumeshawabaini ni wafanyabiashara wakubwa tena wala hawatoki hapa Dar es Salaam, hawa ni wakwepa kodi, wanaamua kutumia nguvu yao ya fedha kuwalazimisha wenzao kugoma tena kwa kuwatishia tumeshawasiliana na polisi kwa hatua za kisheria.”

Naibu Waziri wa Wizara, Saada Mkuya alisema miongoni mwa wafanyabiashara waliogoma wapo ambao hawajui umuhimu wa matumizi ya mashine hizo lakini wamelazimika kujiunga na mgomo kwa kushinikizwa na wenzao.

TRA watoa kauli
Kamishna Mkuu wa TRA, Harry Kitilya alisema kuwa mpango wa kukusanya kodi kwa mashine hizo utabakia palepale na kudokeza kwamba muda wa waliokuwa wanakwepa kodi kulipa umefika.

“Mimi sioni tatizo ni nini, kama elimu tulikwishatoa kwa kada mbalimbali, tena bure, sasa sijui wanachotaka nini! Nadhani wale wanaokwepa kodi ndiyo hao wanaochochea wengine kufanya haya yatokee, lakini utaratibu utaendelea,” alisema Kitilya jana.

Wakubaliana na RC Sadick
Jana, wafanyabiashara hao walikutana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick na kukubali kufungua maduka yao kuanzia leo huku Serikali ikiendelea kushughulikia suala lao. Hata hivyo walisema watasimamisha mgomo wao hadi Desemba wakati Serikali ikitafakari cha kufanya.

Akizungumza mara baada ya kikao hicho kilichoanza saa nne asubuhi na kudumu kwa zaidi ya saa tatu, Sadick alisema: “Tumekutana na TRA pamoja na wafanyabiashara na tumekubaliana wafungue maduka kuanzia kesho (leo) huku Serikali ikitafuta njia ya kufanya kuondoa malalamiko yao.”

Mkuu huyo wa mkoa alisema wafanyabiashara ndogondogo hawahusiki na matumizi ya mashine hizo na kwamba hawatakiwi kuingilia na kuwashawishi wenzao kugoma kwani hilo ni kosa.

Mwenyekiti wa umoja
Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Kariakoo, (UWK), Mathias Makoyo alisema: “Tumezungumza na TRA na mkuu wa mkoa na wametutaka tufungue maduka yetu huku kamati ya wajumbe 20 ikifanya kazi ya kushughulikia suala hili.”

Chanzo; Mwananchi