Na Immaculate Makilika – Maelezo
WIZARA inatekeleza mpango maalumu wa kuboresha huduma ya majisafi na uondoaji wa majitaka jijini Dar es Salaam kupitia mamlaka ya Majisafi na Maji taka Dar es Salaam(DAWASA). Katika utekelezaji wa mpango huo, Serikali inaweka utaratibu wa usimamizi wa ufuatiliaji wa karibu kwa kuzingatia hadidu za rejea zilizopo kwenye mikataba na ratiba za kazi.
Hayo yamesemwa Bungeni mjini Dodoma, wakati Naibu Waziri wa Maji Gerson Lwenge alipokuwa akijibu Swali la nyongeza la John Mnyika (Ubungo) alipouliza maswali kadhaa ikiwemo kwanini mwezi Machi umeshapita bila ya mfumo kukamilisha utekelezaji wake, kwanini utekelezaji wa mpango huo kutoka Ruvu – Kimara. unachukua muda mrefu bila kukamilika pamoja na kasoro za mradi wa mabomba ya wachina.
Akijibu maswali hayo Lwenge alisema utekelezaji wa shughuli za maji zinahitaji ufundi mpana zaidi ndio maana zinachukua muda katika utekelezaji wake, lakini pia sh. bilioni 653 zinatumika katika mradi wa Ruvu juu, Ruvu chini na visima vya mpera.
Naibu huyo aliendelea kwa kusema kuwa Serikali inafanya kazi kubwa ,na vyanzo vya maji vitafanya mabomba ya china yaanze kutumika.
Aidha katika utekelezajio wa sheria za Maji, Wizara inaendelea kubaini mapungufu yaliyopo kwenye Sheria za Maji, Kwa upande wa DAWASA, mapungufu kadhaa yamebainishwa na sasa yako katika hatua mbalimbali za kupitishwa kwenye vikao husika.
Baada ya kukamilika, muswada wa marekebisho ya sheria hiyo utawasilishwa hapa Bungeni. Kwa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira, mapungufu kadhaa yamebainishwa na unaendelea kukusanyua maoni kutoka kwa wadau ili tuwe na uchambuzi wa kina alisema Naibu waziri huyo.