Serikali Yaja na Mbinu Kudhibiti Wizi wa Fedha Kimtandao

Nembo ya Taifa

Immaculate Makilika- Maelezo

SERIKALI imesema kwamba Benki ya NMB inatarajia kuanzisha utaratibu wa kutuma ujumbe wa simu kwa wateja kupitia simu zao (Bank massage) pindi mteja atakapofanya muamala ili mwenye akaunti kuridhia/kukataa au kufahamu kuwa kipindi hicho akaunti yake inatumika kutoa fedha.

Aidha, Serikali imefafanua kuwa imezitaka benki zote kutumia teknolojia ya kisasa ya (Euro Mastercard Visa-EMV Compliant) ambayo hutumia mfumo wa “chip based” na kuachana na mfumo wa kizamani unaotumia “magnetic stripe”. Ambao kwa sasa umepitwa na wakati na ni rahisi kwa wahalifu kuuchezea na kuiba fedha za wateja.

Hayo yamesemwa leo Bungeni mjini Dodoma wakati Naibu Waziri wa  Fedha, Saada Mkuya alipokuwa akijibu swali la Kidawa Hamid Saleh (Viti Maalum – CCM) alipouliza je, Serikali ina mkakati gani wa kupambana na matatizo ya wizi wa Mabenki kwa njia ya mtandao.

Alisema kupitia Benki Kuu ya Tanzania imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali katika juhudi za kupambana na tatizo la wizi kwa njia ya mtandao.

Aidha Naibu waziri alisema hatua zingine za kukabiliana na tatizo hili la mabenki ni kuweka mfumo wa “Anti- Skimming  Devices ambapo mfumo huu unazuia mwizi kugundua namba ya siri ya mteja(PIN), na kwa upande wa Benki ya NMB imeamua kusimamisha utaratibu wa “swapping” uliokuwa unatekelezwa na kampuni ya simu ya Airtel.

Katika swali la nyongeza Kidawa aliuliza pia kama Serikali imewapa adhabu yeyote wafanyakazi wa NMB na Airtel waliobainika kuhusika na upotevu wa fedha za wateja na je kama Benki ya NMB itarejesha fedha hizo kwa wateja?

Mkuya alijibu maswali hayo kwa kusema kuwa bado hajajua namna gani NMB na Airtel imewaadhibu wafanyakazi wak, isipokuwa kuhusu kurejesha fedha kwa wateja  ndio NMB  inafanya hivyo. Aidha Naibu waziri huyo aliendelea kwa kusema  Serikali inakamilisha sheria ya wizi kwa njia ya mtandao (Cyber Crime Act) ambayo itasaidia kupunguza tatizo hilo.