Serikali Yafafanua Ukomo wa Madaraka ya Rais na Mawaziri

Nembo ya Taifa la Tanzania

Nembo ya Taifa la Tanzania


SERIKALI imetoa ufafanuzi kuhusu ukomo wa madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mwisho wa uhai wa Baraza la Mawaziri kwa kadri Tanzania inavyoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaofanyika Jumapili, Oktoba 25, mwaka huu, 2015.

Taarifa iliyotolewa, Oktoba 21, 2015, Ikulu, Dar es Salaam na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Yohana Sefue imesema kuwa Serikali imetoa ufafanuzi huo kuwasaidia wananchi kuelewa maelekezo na matakwa ya Katiba na Sheria kuhusu ukomo wa madaraka ya Rais na mwisho wa Baraza la Mawaziri kufuatia mijadala ya karibu katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Taarifa hiyo imekariri Ibara ya 42(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo inasema kuwa ukiacha sababu nyingine, mtu anayechaguliwa kuwa Rais atashika madaraka ya kiti cha Urais hadi Rais Mteule atakapoapishwa.

Ibara hiyo ya 42(3) inasema: ”Mtu anayechaguliwa kuwa Rais, atashika kiti cha Rais hadi – (a) siku ambako mtu anayemfuatia katika kushika kiti hicho atakula kiapo cha Rais.”

Taarifa hiyo imesema: “Hivyo, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais anaendelea kuwa Rais, akiwa na madaraka na mamlaka yote na kamili yanayoambatana na nafasi hiyo, hadi Rais Mteule anakapokula kiapo cha Urais. Hivyo, ni vyema wananchi waelewe kuwa hakutatokea wakati wowote ambapo hakuna Rais na Amiri Jeshi Mkuu mwenye mamlaka kamili na aliye tayari kuyatekeleza mamlaka hayo. Lengo ni kuhakikisha kuwa haitokei wakati wowote nchi yetu ikakosa Rais na Amiri Jeshi Mkuu.”

Imesisitiza taarifa hiyo: “Madaraka na mamlaka ya Rais yapo, na hayapugui kwa namna yoyote ile, hata baada ya Uchaguzi Mkuu, mpaka Rais Mteule atakapoapishwa.”

Kuhusu ukomo wa Baraza la Mawaziri, taarifa imefafanua kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 57(2) ya Katiba, Waziri na Naibu Waziri ataendelea kushikilia mamlaka ya nafasi yake hadi, ukiacha sababu nyingine, Rais mteule atakapoapishwa.

Ibara hiyo 57(2) inatamka: “Kiti cha Waziri au NaibuWaziri kitakuwa wazi litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo – (f) Ukiwadia wakati wa Rais Mteule kushika madaraka ya Rais, basi mara tu kabla ya Rais Mteule hajashika madaraka hayo.”

Taarifa hiyo imeongeza kuwa Mawaziri na NaibuMawaziri wanaendelea kushikilia nafasi zao, wakiwa na madaraka na mamlaka kamili yanayoambatana na nyadhifa zao hadi mara tu kabla ya Rais Mteule hajashika madaraka.

Imemalizia taarifa hiyo: “ Naomba vyombo vya habari, vyenye jukumu la kuelimisha jamii, kuwaelewesha Watanzania kuhusu utaratibu huu wakubadilishana madaraka kati ya awamu moja ya uongozi wa nchi na nyingine. Madaraka na mamlaka ya Rais yapo, na hayapungui kwa namna yoyote ile, hata baada ya uchaguzi Mkuu mpaka Rais Mteule atakapoapishwa.”