SERIKALI imeanza kujibu hoja za tuhuma za uwepo wa uchotwaji wa fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow takribani sh. bilioni 306 zinazodaiwa kuchotwa na watu binafsi, viongozi wa siasa, watendaji wa Serikali pamoja na viongozi wa dini, kwa mujibu wa ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyowasilishwa jana bungeni mjini Dodoma.
Akijibu hoja hizo leo mjini Dodoma Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesisitiza kuwa fedha zinazodaiwa kuchotwa si mali ya Seriali bali ni za kampuni ya IPTL na walizitoa baada ya kujiridhisha kuwa si mali ya umma na hivyo hazina madhara kwa taifa.
Alisema madai ya Kamati ya PAC kuwa fedha hizo zimo na za Serikali hayana ukweli wowote na kitendo ilichokifanya ni kulidanganya bunge na umma wa Watanzania jambo ambalo si la kiungwana. Waziri huyo ambaye alikuwa akijibu hoja hizo kwa kujiamini alisema wizara yake haijakiuka taratibu zozote wala kufanya uzembe bali imesaidia kuokoa kuokoa takribani sh. bilioni 95 kwa kufanikisha kumalizika kwa mgogoro huo kati ya IPTL na Tanesco.
Madai kwa IPTL Serikali ilihakikisha inachukua kinga kutoka IPTL ili kama kukijitokeza madai yoyote IPTL itawajibika yenyewe, kinga hiyo ilithibitishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Oktoba 27 2013. Profesa Sospeter Muhongo katika maelezo hayo alisema hata kama Mamlaka ya Mapato (TRA) inadai kodi yoyote kutokana na fedha hiyo iende IPTL ilipwe.
Madai yanayotolewa na Tanesco ya kwamba wanaidai IPTL sh. bilioni 321 msingi wake ni kwamba mtaji wa IPTL ni dola za Kimarekani milioni 100, dhana ambayo wanaamini Dola za Marekani milioni 33.1 ndizo gharama za uwekezaji wa mtambo wa IPTL Tegeta. Hadi mara ya mwisho unafanyika ukaguzi na Tanesco kuridhia kabla ya mbia wake kulipwa Tanesco ilikuwa ikidaiwa sh. bilioni 275.20, fedha ambazo ni pungufu ya sh. bilioni 95 ya madai hayo.
Hata vitabu vya ukaguzi wa mahesabi ya Tanesco havioneshi kuwepo kwa madai hayo. Tanesco kwa kushirikiana na IPTL ilifanya uhakiki Oktoba 09, 2013 ili kujua madai halali ya IPTL kabla ya kufanya malipo takwimu za RITA zilionesha kuwa deni alilokuwa akidaiwa Tanesco na IPTL ni sh. bilioni 370.70.
Profesa Sospeter Muhongo alisema vielele vyote vya kuonesha ukweli wa suala la akaunti ya escrow vipo na vitatolewa kwa wabunge ili ukweli ujulikane na kumaliza uzushi uliopo. Katika hotuba yae akijibu hoja za Kamati ya PAC waziri huyo alikatishwa katishwa kwenye hotuba kutokana na kuibuka kwa mvutano bungeni ambayo ilizua kelele kwa baadhi ya wabunge na hata alipoitimisha. Baadhi ya wabunge hasa upinzani walipinga Muhongo kuongeza maneno ambayo hayakuwa katika majibu yake.
Jana Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), iliwasilisha bungeni ripoti ya uchunguzi wa uporaji wa takribani bilioni 306 zinazodaiwa kuchotwa katika akaunti ya Tegeta Escrow zikiwemo fedha za Seriali ya Tanzania, huku ikitoa mapendekezo Waziri Mkuu wa Tanzania ajiuzulu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake.
Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe bungeni, alisema kamati hiyo imethibitisha kuwa utaratibu mzima uliyotumika katika utoaji wa fedha hizo umegubikwa na mazingira ya rushwa na mchezo mchafu uliosaidia uchotwaji wa fedha kiasi cha bilioni 306 kuporwa kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na kutakatishwa na benki kadhaa nchini na nyingine za nje ya nchi. Fedha hizo zilikuwa ni mali ya Serikali na mbia wake kampuni ya IPTL.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe akiwasilisha mapendekezo ya Kamati ya PAC bungeni alisema baada ya kupitia vielelezo vyote vilivyopo kwenye ripoti ya CAG kamati ya bunge imejiridhisha pasipo na shaka kuwa Waziri Mkuu (Mizengo Pinda) alikuwa na taarifa zote kuhusiana na mchakato mzima wa uporaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow na ndio maana alikuwa akitetea bungeni hazikuwa za Serikali.
Sehemu ya fedha zilizokuwemo katika akaunti hiyo, Tanesco walikuwa na kiasi cha sh. bilioni 142 huku Wizara ya Nishati na Madini ilikuwa na sh. bilioni 40, na kodi ya ongezeko la thamani iliyopotea baada ya fedha kutolewa kiasi cha sh. bilioni 23 mali ya TRA.
“…Ushahidi ulioletwa unaonesha kuwa Waziri Mkuu alikuwa akipata taarifa za jambo hili na kamati imesikitishwa kuona kuwa hakuchukua uamuzi wowote wa kuzuia muamala huu usifanyike maamuzi au maelekezo yoyote ya kuzuia muamala huu usifanyike ilhali ana mamlaka kwa mujibu wa Katiba ya nchi…,” alisema Filikunjombe.
“…Waziri Mkuu atakuwa na madaraka ya juu ya udhibiti na usimamiaji utekelezaji wa siku hadi siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Muungano…kamati ilijiuliza ni nini matamko ya mara kwa mara bungeni na nje ya bunge kuhusiana na suala hili kupotosha kwamba hazikuwa fedha za Serikali.
Katika taarifa hiyo kamati imebaini pia Wizara ya Nishati na Madini kupitia kwa Katibu Mkuu wake (Elihakimu Maswi), haikufanya jitihada za kutosha kuhakiki mauziano ya hisa kama alivyokuwa imeomba hapo awali yamefanyika kitaratibu na muhusika kutambulika kisheria.
“Uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini ilishindwa kutimiza wajibu wake ipasavyo kuhakikisha fedha za umma zinalindwa hivyo kufanikisha uchotaji wa fedha katika akaunti hiyo hivyo kuwasaidia wizi wa fedha hizo wahusika. Wahusika katika fedha hizo ni Serikali na IPTL,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imebaini kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Elihakimu Maswi aligoma fedha hizo kutolewa lakini ndani ya siku nne baadaye alibadili msimamo na kuruhusu fedha zilizopo katika akaunti ya Escrow kutolewa jambo ambalo linazua mashaka kwa mtumishi huyo wa Serikali.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa malipo yote ya shs bilioni 167 na Dola za Kimareani milioni 22 yaliyokuwa katika akaunti hiyo yalilipwa kwa kampuni ya PAP na sio IPTL kupitia banki ya Stabic Novemba 27, 2013.
Walionufaika katika sehemu ya mgao wa fedha uliolipwa wapo viongozi wa siasa, majaji, viongozi wa madhehebu ya dini na watumishi wengine wa Serikali jambo ambalo limeibua mashaka ya uhusiano wa watu hao kulipwa mabilioni ya fedha toka kwa mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing, Rugemalira.
Baadhi ya watu walienda kuchukua fedha katika benki tajwa wakiwa na mifuko ya rambo, maboksi, sandarusi na maguni. Na kutokana na muamala uliyofanyika tarehe 6 Februari, 2014 katika benki ya Mkombozi kiasi cha shilingi bilioni 3.3 na muamala wa benki ya Stanbic uliofanywa tarehe 23, Januari 2014 kiasi cha fedha taslimu sh. bilioni 73 ziligawiwa kwa watu kinyume na utaratibu wa Benki Kuu (BoT).
Kamati imependekeza Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya IPTL na PAP, Harbinder Singh Sethi kufikishwa Mahakamani alifanya udanganyifu kwa kushirikiana na viongozi waandamizi wa Serikali na kuwasilisha nyaraka feki za kuonesha kuwa ni mmiliki wa hisa 70 za na kufanikisha kuchota kiasi cha shilingi bilioni 306 kutoka BoT. Seti alikiuka sheria za kodi na kujipatia mali asiyostahili, kutakatisha fedha haramu na kuhujumu uchumi wa nchi.
Kamati imeitaka Takukuru na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Nchini (DCI) kumkamata, Harbinder Singh Sethi na kumfungulia mashtaka mara moja ya ukwepaji wa kodi, utakatishaji fedha haramu na wizi alioufanya katika sakata la uporaji wa fedha hizo. Aidha Kamati imeshauri mamlaka husika kuhakikisha inatumia sheria zilizopo kuhakikisha Singh Sethi anarejesha fedha zilizoporwa BoT.
Kamati pia imewataka waliopata mgao wa fedha wazirejeshe kwa kuwa kiasi hicho ni sehemu ya fedha ya Serikali na walio viongozi wa umma wachunguzwe kama walikiuka sheria ya maadili ya umma ambayo inawataka kutoa taarifa ya zawadi wanazopokea. Imependekeza pia kuvuliwa nyadhifa zao za kuchaguliwa na uteuliwa kutokana na makosa waliyoyafanya ikiwa ni pamoja na kufilisiwa kufidia fedha walizochota na kushtakiwa.