Serikali Yaandaa Utaratibu Ufuatiliaji Miradi Inayozinduliwa Katika Mbio za Mwenge

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Ali Nassoro Lufunga akizungumza na viongozi na waratibu wa mbio za Mwenge kutoka maeneo mbalimbali nchini kuhusu maandalizi ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2013. Mkoa wa shinyanga ulikuwa mwenyeji wa kilele cha mbio za Mwenge mwaka 2012. (Picha na Aron Msigwa)

Na Aron Msigwa–MAELEZO, Zanzibar

SERIKALI inaandaa utaratibu wa kufuatilia maendeleo ya miradi inayozinduliwa wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru ili kuhakikisha miradi hiyo inakua endelevu na kuwanufaisha wananchi.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini Zanzibar na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana nchini kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel wakati akitoa tathmini ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2012 na maendeleo ya miradi iliyozinduliwa wakati wa mbio hizo, kwenye mkutano wa viongozi na waratibu wa mbio za Mwenge kutoka maeneo anuai nchini.

Alisema serikali ina wajibu wa kufuatilia kwa karibu miradi yote iliyozinduliwa na Mwenge wa Uhuru 2012 katika Halmashauri za wilaya, manispaa na Miji ili kuhakikisha kuwa gharama kubwa iliyotumika wakati wa uanzishaji na ujenzi wa miradi hiyo inawanufaisha wananchi kutoka kizazi kimoja hadi kingine ili kutunza hadhi na heshima ya Mwenge wa Uhuru.

Alisema mbio za Mwenge wa uhuru zimezindua miradi mingi nchini yenye thamani ya mabilioni ya fedha na kuongeza kuwa si dhamira ya Serikali kuona kuwa mwenge wa uhuru unatumika tu kuzindua miradi ya maendeleo bali kuhakikisha uendelevu wa miradi hiyo.

“Mbio za Mwenge wa Uhuru kila mwaka zinazindua miradi mikubwa inayogharimu fedha nyingi, lazima tufanye tathmini ya miradi yote inayozinduliwa na hatutapenda kuona mwenge unatumika tu kuzindua miradi kwa maana sherehe, tutapenda kuwa na taarifa za maandishi juu ya hali ya miradi hiyo ili itolewe kwenye tathmini ya mbio za mwenge kwa miaka inayofuata” amesisitiza Prof. Gabriel.

Aliongeza kuwa utaratibu huo wa ufuatiliaji utawahusisha wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri zote ambazo Mwenge wa Uhuru utazindua miradi katika maeneo yao ili kutoa fursa kwa wananchi kuendelea kunufaika na miradi hiyo na mbio za Mwenge wa Uhuru.

Aidha Prof. Gabriel ametoa wito kwa wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa miradi yote inayozinduliwa na Mwenge wa Uhuru inapewa kipaumbele katika usimamizi na ufuatiliaji.

Kwa upande wake Bw. Wito Mlemelwa mmoja wa wakimbiza Mwenge wa Uhuru mwaka 2012 akitoa taarifa ya tathmini ya mbio za Mwenge kwa wajumbe wa mkutano huo kwa niaba ya kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa ametoa wito kwa watendaji na viongozi wa maeneo mbalimbali kuhakikisha kuwa miradi yote inayotarajiwa kuzinduliwa na Mwenge wa Uhuru inakamilishwa kwa ubora na viwango ili kuepuka kukataliwa.

“Natoa wito kwa watendaji wa maeneo mbalimbali wawe makini wahakikikishe kuwa miradi yote inayozinduliwa na Mwenge wa uhuru inakidhi ubora na viwango vilivyowekwa kulingana na gharama halisi ya fedha iliyotumika kwa sababu Mwenge wa Uhuru hautahusika kuzindua miradi iliyo chini ya kiwango,” amesisitiza Bw. Mlemelwa. Katika kipindi cha mwaka 2012 mbio za Mwenge wa Uhuru nchini zilizidua miradi 273 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 158.