SERIKALI imeandaa mafunzo ya majadiliano ya mikataba kwa wataalamu mbalimbali ili kuwapa mbinu za kuendesha mikataba ya kibiashara inayohusu rasilimali za nchi kwa manufaa ya Watanzania. Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju wakati wa ufunguzi wa semina ya wiki moja kuhusu majadiliano ya mikataba inayoendelea kwenye hoteli ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam iliyohusisha maofisa waandamizi wa Serikali kutoka maeneo tofauti.
“Nchi yetu hivi sasa iko katika mikakati ya kutumia rasilimali zilizopo kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania kupitia Sheria ya Ubia ya Pamoja kutoka sekta binafsi (PPP) kwa kuwahusisha wawekezaji wa ndani na nje. Mafunzo haya yawatawasaidia kufanya kazi kwa ufanisi na kuweza kukabiliana na kampuni kubwa zenye uwezo wa kifedha, katika mikataba inayohusu madini, mafuta gesi, nishati, Kilimo kwanza ili kuhakikisha tunapata faida,” alisema Masaju.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa Dira ya Maendeleo ya Taifa ifikapo mwaka 2025 Tanzania iwe nchi nyenye kipato cha kati. Hivyo nchi yetu bado inawahitaji wataalamu kwenye maeneo hayo.
Alisema mafunzo hayo yamehusisha mawakili tisa kutoka katika ofisi hiyo na wengine toka taasisi mbalimbali za umma. Aliwataka washiriki wasemina hiyo kutumia mafunzo hayo kwa ajili ya kubadilishana mawazo na kupeana uzoefu juu ya suala hilo. Mafunzo hayo yameandaliwa na Taasisi ya Uongozi.