Na Eleuteri Mangi-MAELEZO Mtwara
RASILIMALI za gesi asilia, mafuta na madini zilizopo mikoa ya Lindi na Mtwara ni kwa neema, ukarimu, ufadhili na baraka za Mwenyezi Mungu alizoipatia Tanzania hivyo ni vema zitumike kwa manufaa ya wanachi wote bila ubaguzi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mgeni rasmi Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikani Tanzania Dk. Jacob Chimeledya alipokuwa akifungua Kongamano la Viongozi wa Dini leo katika ukumbi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mjini Mtwara.
Kongamano hilo la viongozi wa dini liliongozwa na kauli mbiu iliyosema “Rasilimali zetu za gesi asilia, mafuta na madini kwa amani na maendeleo ya Tanzania”.
Lengo la kongamano la viongozi wa dini lilikuwa ni kupata elimu juu ya rasilimali hizo muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi kwa minajili ya haki, upendo na amani kwa kuzingatia sera na taratibu za Serikali kwa maslahi ya wananchi wote.
“Pamoja na sheria na sera za rasilimali za gesi, mafuta na madini zilizopo nchini, ni lazima ziongozwe na misingi muhimu ya taifa letu” alisema Askofu Dk. Chimeledya.
Dk. Chimeledya aliitaja misingi hiyo kuwa ni pamoja na haki ya kila mtanzania, ukweli juu ya sera mipango na mikakati bora, mshikamano wa jamii, kujali maslahi ya wote na ushirikishwaji wa jamii zilizo katika maeneo yanayozunguka sehemu zilipo rasilimali mbalimbali nchini.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi alisema kuwa Serikali kupitia Wizara yake ipo tayari kuendelea kushirikiana na viongozi wa dini na wanachi wote ili kuendelea kusukuma mbele maendeleo ya nchi kwa manufaa ya watu wake.
“Gesi ni ukombozi ni ukombozi na itatusogeza mbele ambapo italinufaisha taifa katika Nyanja mbalimbali, viwandani, majumbani na ndani ya nchi hata nje ya nchi” alisema Maswi.
Kugunduliwa kwa gesi mikoa ya Lindi na Mtwara kumefungua milango ya kujengwa viwanda mabalimbali ambavyo vinatajiwa punguza tatizo la ajira katika mikoa hiyo na nchi nzima kwa ujumla. Miongoni mwa viwanda vya saruji vinavyoendelea kujengwa ni Dangote kilichopo Mtwara na Meis kilichopo mkoani Lindi.
Katibu Mkuu Maswi ametoa rai kwa watanzania wenye uwezo wa kuwekeza kupitia viwanda wafikirie kuwekeza juu ya viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotumia malighafi zinazotokana na mabaki gesi baada ya kuchakatwana ikiwemo viwanda vya mbolea, plastiki, chupa na nguo.
Viongozi hao wa dini walipata fursa ya ziara ya kutembelea mitambo ya kusafisha gesi na visima vya gesi Mnazi Bay eneo la Msimbati na eneo la juenzi wa mitambo ya kusafisha na kuchakata gesi kilichopo eneo la Madimba mkoani Mtwara.
Kongamano kwa viongozi wa dini ni la siku mbili ambapo linawashirikisha viongozi wa dini mbalimbali za kikristo na kiislam kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara pamoja na viongozi na watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na madini na mashirika yaliyo chini yake ya TANESC, TPDC NA REA.
Kongamano hilo ni muendelezo ulitokana na kongamano kama hilo lililofanyika Januari 2014 jijini Dar es salaam ambapo wajumbe kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara waliona kuna haja wao kama wadau wa gesi, mafuta na madini wapate elimu kama hiyo kwa manufaa ya wanachi wa mikoa yao na nchi nzima.