BUNGE la Ugiriki limeidhinisha mpango mpya wa serikali ya nchi hiyo wa kupunguza matumizi yake ili kukabiliana na mzozo wa madeni unaokumba taifa hilo.
Kura kuhusu mswada huo ambao utapunguza matumizi ya serikali na kuongeza viwango vya ushuru, imejiri baada ya ghasia na maandamano yaliyofanywa na wafanyikazi wa umma kupinga mikakati hiyo.
Mabomu ya petroli na mawe yalirushwa wakati wa maandamano hayo ambayo ndiyo makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo huku maelfu ya raia wa nchi hiyo wakishiriki.
Bunge hilo la Ugiriki linatarajiwa kujadili mswada huo kwa mara nyingine hii leo, kabla ya kuipigia kura mara ya mwisho, kabla kuwa sheria.
Mikakati hiyo ni sehemu ya mpango wa kunusuru taifa hilo kutokana na mzozo wake wa madeni, lakini waandamanaji wanasema mpango huo utapelekea taifa hilo kujilimbikizia madeni zaidi.
-BBC