WASHINGTON
KUWA kiongozi wa dunia huru (the leader of the free world) ni mpango wenye gharama, na gharama zake hazikomi siku unapofungasha virago vyako kutoka Jumba Jeupe (White House). Serikali ya Marekani imetumia takribani Mil $3.7 mwaka jana kwa marais wake wastaafu, yaani, Jimmy Carter, George H.W. Bush, Bill Clinton, na George W. Bush (Maarufu kama Bush mtoto), hii imegundulika kutokana na uchunguzi uliofanyika na kutolewa hivi karibuni na kitengo huru cha Bunge chenye kutoa huduma za uchunguzi wa serikali kwa jamii.
Kiwango kilichotajwa, kinajumuisha kiinua mgongo, marupurupu, na marejesho ya wafanyakazi wa ofisi za marais hao wastaafu. Pamoja na hayo, serikali bado inabeba gharama za usafiri, ofisi, na posta (postage).
Katika taarifa hiyo, Rais George W. Bush (mtoto) anatajwa kama ndio rais aliyekuwa na gharama kubwa kuliko wote mwaka jana kwa kufikia kiwango cha Mil $1.3. Wengi wanahoji uhalali wa marais hawa kuendelea kuwa umiza walipa kodi kiasi hiki, ukizingatia kwamba marais wastaafu wa Marekani ya leo wana fursa mbalimbali za kutengeza pesa. Fursa hizo ni kama kuandika vitabu, kuzungumza sehemu mbalimbali nje na ndani ya Marekani, na mengineyo. Hii ukiachilia mbali kiinua mgongo cha $296,000, ambacho marais hao wastaafu wanalipwa na serikali kwa mwaka.
Baadhi ya Wabunge wanataka sheria ibadilishwe ili marais wapewe kiwango maalum cha matumizi pindi wanapo staafu, ili kuwapunguzia walipa kodi mzigo haswa katika kipindi hiki kigumu kiuchumi, ambapo serikali ya Marekani ina lazimika kupunguza matumizi katika bajeti yake.
Source: Associated Press (AP)
Tafsiri: dev.kisakuzi.com