Na Frank Mvungi, MAELEZO
SERIKALI imeendelea kuimarisha umoja, amani na utulivu miongoni mwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi cha miaka kumi. Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Angelina Madete wakati wa mkutano na vyombo vya habari jijini Dar es salaam.
Mhandishi Madete alisema kuwa suala la muungano ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya awamu ya nne kwa dhumuni la kuimarisha umoja na utulivu nchini.
“Serikali ya awamu ya nne inajivunia uimarikaji wa Umoja, amani na utulivu miongoni mwa wananchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani ilikuwa ni moja ya kipaumbele kilichowekwa na serikali hii katika kipindi cha miaka Kumi ya Uongozi wa Rais Dk. Jakaya Kikwete.” Alisema Mhandisi Madete.
Mhandishi Madete aliongeza kuwa Taasisi za Muungano kama Ulinzi na Usalama, Uhamiaji na Uraia, Fedha, Sarafu na Mawasiliano zimeendelea kuimarika kwa kutoa huduma bora kwa wananchi katika kipindi cha Serikali ya awamu ya nne.
Akifafanua Madete amesema katika kipindi cha awamu ya nne wananchi wa pande zote mbili za muungano wameendelea kunufaika na shughuli za kiuchumi na kuongeza ajira kupitia utekelezaji wa program za maendeleo ikiwemo mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF), Progamu ya usimamizi wa Bahari na Pwani (MACEMP) na mradi wa kutoa mikopo kwa ajili ya miradi midogomidogo (SELF).
Miradi mingine ni program ya maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP), mradi shirikishi wa program za maendeleo ya kilimo( PADEP) na program yamaendeleo ya Mileninia ambayo kwa pamoja imewanufaisha wananchi kwa kuwaletea maendeleo endelevu.
Mafanikio mengine ni ujenzi wa majengo ya Taasisi za Muungano ikiwemo kukamilika kwa ujenzi wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mtaa wa Lithuli, Dar es salaam,awamu ya pili ya ujenzi wa ofisi ya Makamu wa Rais Tunguu-Zanzibar umekamilika kwa kiwango kikubwa.
Pia ujenzi wa Tawi la Benki Kuu lililopo Gulioni Zanzaibar umekamilika ambapo majengo mengine yaliyojengwa ni pamoja na uhamiaji, Makao makuu na Ofisi za BungeTunguu na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH). Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kuratibu shughuli za Muungano na kudumisha ushirikiano kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Pia itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa Muungano kwa wananchi wote.