*Maisha yake alipigania Muungano na Muundo wa Serikali mbili
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa sherehe za leo za Kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, zingekuwa zinamkejeli moja kwa moja Mwalimu kama Katiba Inayopendekezwa ingekubali pendekezo la Serikali Tatu.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa hajui Watanzania wangesema nini katika sherehe za mwaka huu wa Kumbukumbu hiyo kama Tanzania ingekuwa na Katiba Inayopendekezwa ingekuwa imesisitiza Muungano wa muundo wa Serikali tatu.
Vile vile, Rais Kikwete amesema kuwa Muungano wa Serikali Mbili ndiyo hasa urithi mkuu ambao Mwalimu Nyerere aliwaachia Watanzania na wana budi kuendelea kuulinda na kuuthamini urithi huo. Rais Kikwete alikuwa anazungumza na Taifa leo, Jumanne, Oktoba 14, 2014, kwenye Sherehe ya Kuzima Mwenge wa Uhuru, Kumbumbuku za Mwalimu Nyerere na Kumalizika kwa Wiki ya Vijana iliyofanyika kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora ambao ulijaa maelfu kwa maelfu ya wananchi kuasdhimisha matukio hayo.
Rais Kikwete amewaambia wananchi kuwa ni jambo mwafaka na faraja kabisa kuwa Katiba Inayopendekezwa imesisitiza ubora wa kuendelea na Muungano wa Serikali mbili alizoziasisi Mwalimu Julius Nyerere akiwa na Mzee Abeid Amani Karume. Amesema Rais Kikwete: “Bila shaka mtakumbuka jinsi Mwalimu alivyoupigania muundo huu kwa nguvu zake zote wakati wa uhai wake. Hatuna budi kulipongeza Bunge Maalum la Katiba kwa kumuenzi kwa dhati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kudumisha urithi wake mkuu.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Sijui tungesema nini katika Sherehe za mwaka huu kama ndiyo tungekuwa na Katiba Inayopendekezwa yenye Muungano wa muundo wa Serikali Tatu?”
“Sherehe za mwaka huu ni spesheli kweli kweli kwani zinafanyika siku chache baada ya Bunge Maalum la Katiba kukamilisha kazi na kukabidhi Katiba Inayopendekezwa, Katiba ambayo siyo tu ni nzuri lakini ni Katiba bora. Nimebahatika kuisoma Katiba Inayopendekezwa na naendelea kuisoma kwa sababu ina mambo mengi mazuri. Kwa kweli ni Katiba bora kuliko hii tuliyonayo sasa yaani Katika ya Mwaka 1977.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Hii ndiyo yenyewe hasa. Hii ndiyo Katiba ya Wananchi. Ni Katiba inayotambua na kuimarisha tunu za taifa letu na mambo mazuri ya huko tulikotoka na hapa tulipo. Ni katiba inayorekebisha upungufu uliopo sasa na kuweka mifumo mizuri inayoendana na wakati tulionao sasa na huko mbele tuendako. Kwa lugha nyepesi ni Katiba inayojibu changamoto zetu za leo na kesho.”
Amewaambia wananchi Rais Kikwete: “Katiba Inayopendekezwa inatokana na ushirikishwaji mpana wa wananchi wa Tanzania walioko ndani na nje ya nchi. Hata Watanzania waishio nje ya nchi walikuwa na uwakilishi ndani ya Bunge Maalum la Katiba. Ndiyo maana haki na maslahi ya makundi yote yametambuliwa na kupewa nafasi yake stahiki.”