SERIKALI imetoa tamko kuhusu utafiti wa chanjo ya ugonjwa wa Ukimwi unaoendelea nchini, ikisema: “Matokeo yake yanatia matumaini.” Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja alisema jana kuwa chanjo hiyo ni majaribio ya kimaabara yanayohusu wanyama (nyani) kabla ya matumizi kwa binadamu.
Alisema majaribio hayo yalifanywa na Taasisi ya Mzio na Magonjwa ya Kuambukiza ya Marekani, Programu ya Utafiti wa Ukimwi ya Jeshi la Marekani yalionyesha kuwa, kima waliopata chanjo hiyo walikingwa dhidi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi. “Pamoja na matokeo hayo mazuri ni vyema jamii ikaelewa kwamba majaribio kama haya hayajafanyika kwa binadamu,” alisema Mwamwaja.
Mwamwaja alisema bado wanaendelea na utafiti wa chanjo ya Ukimwi nchini na kwamba mchakato wa kuainisha matokeo unaendelea. Alisema utafiti huo unafanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUHAS) na mtu wa mwisho alichanjwa Januari mwaka huu.
Alisema majaribio hayo yanalenga kuainisha usalama na uwezo wa kujenga kinga ya binadamu dhidi ya Virusi vya Ukimwi. “Hata hivyo, jamii inapaswa kuelewa kwamba majaribio yanayoendelea nchini yapo katika hatua za awali hivyo tathmini ya uwezo wa kutoa kinga dhidi ya Virusi vya Ukimwi haijafanyika hadi sasa,” alisema Mwamwaja. Alisema majaribio ya awali yalifanywa Sweden kabla ya kuanza nchini na kwamba lengo ni kuendeleza tathmini ya usalama na ubora wa chanjo hiyo ya majaribio.
Aliitaka jamii kuendelea kutumia njia na mikakati ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Ukimwi kama wataalamu wa afya wanavyoshauri na kusisitiza kuwa hadi sasa hakuna chanjo wala dawa ya kutibu ugonjwa huo iliyothibitishwa kitaalamu. Sera ya Ukimwi Katika hatua nyingine; Serikali imeunda jopo la wataalamu kuchunguza na kutengeneza sera itakayowezesha Tanzania kunufaika na matokeo ya tafiti za kutafuta chanjo na tiba ya Ukimwi. Miongoni mwa matokeo hayo ni uwezo wa kuzuia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) bila kondomu, uliofanywa na Chuo Kikuu cha Tiba cha Johns Hopkins, Marekani.
Katika utafiti huo, chuo hicho kilibaini kuwa matumizi ya ARV yanaweza kutumika kama njia ya kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa waathirika kwenda kwa wapenzi wao ambao hawajaathirika kwa asilimia 95 wanaposhiriki ngono bila kondom. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda alisema Serikali tayari imepokea matokeo ya utafiti huo na kinachofanyika sasa ni wataalamu wake kufanya tathmini na kuunda sera.
“Tulipata taarifa hiyo wakati nikiwa Dodoma (Bungeni) kwa sasa nimerejea ninatarajia kukutana na wataalamu wangu kuona hatua za kuchukua,” alisema Dk Mponda mwishoni mwa wiki iliyopita… “Tunataka tufanye tathmini na tuwe na sera ya Taifa katika mpango huo.”
Alisema kuwapo kwa sera hiyo, kutaiwezesha Serikali kuwa na mpango wa tathmini ya kiwango gani ambacho Tanzania imeweza kufanikiwa tangu mpango wa matumizi ya ARV uanze nchini mwaka 2008 na nini kifanyike ili kupunguza zaidi kasi ya maambukizi.
Afrika Kusini wajipanga
Serikali ya Afrika Kusini tayari imeweka mkakati wa kutumia matokeo ya utafiti huo, kukabiliana na maambukizi mapya katika taifa hilo lenye kasi kubwa ya maambukizo kuliko mengine duniani. Mmoja wa wataalamu wa afya wa nchi hiyo, Dk Brian Williams alisema tayari wamefanya tathmini na kuona baada ya miaka mitano watakuwa wamefanikiwa kuyakabili maradhi hayo.
Dk Willams alisema Afrika Kusini ina waathirika milioni sita na kwamba ni asilimia 30 tu wanaopatiwa tiba ya ARV. “Ili kuwagharimia waathirika hao itabidi tutumie Dola za Marekani kati ya milioni mbili hadi tatu (Sh3.2 trilioni hadi 4.8 trilioni) kununua dawa za ARV kwa mwaka,” alisema Dk Williams akiwa Marekani, hivi karibuni.
Kutokana na uzoefu wake, Dk Williams alisema utafiti huo utawasaidia waathirika kuwa katika mazingira mazuri ya kupatiwa chanjo ambayo ipo mbioni kupatikana. Ugunduzi wa Hopkins Katika utafiti huo wa matumizi ya ARV, ilibainika kuwa mtu ambaye anatumia dawa hizo za kupunguza makali, anaweza kufanya tendo la ndoa bila ya kutumia kondomu na mtu ambaye hana Ukimwi na asimwambukize kwa asilimia 95.
Mkuu wa Mtandao wa Maabara za Kuchunguza VVU katika chuo hicho, Profesa Susan Eshleman alisema kwenye ripoti ya ugunduzi huo kuwa wamebaini kuwa ARV sasa zinaweza kutumika kama sehemu ya kuzuia maambukizi. “Huu ni ugunduzi wa kustajabisha,” alisema Profesa Eshleman:
“Matokeo haya yameleta mapambazuko mapya katika sayansi ya kuzuia maambukizi na inawaweka watafiti kwenye mazingira mazuri zaidi ya kupata suluhisho la kukabiliana na maradhi haya.”
Alisema utafiti huo walioupa jina la HPTN 052 waliufanya kupitia maeneo mbalimbali ya dunia hasa yenye kasi kubwa ya maambukizi kama vile Afrika, Brazili, India na Thailand. Kwenye ripoti hiyo ambayo pia ilichapishwa kwenye jarida maarufu la kisayansi linaloitwa Science, watafiti hao wanasema kwamba mtu anapotumia ARV, hufikia wakati fulani wingi wa virusi mwilini hupotea kiasi kwamba anakuwa karibu sawa na yule ambaye hajaambukizwa. “Jambo la msingi katika utafiti huu ni kwamba dawa hizi za ARV zinapotumiwa kikamilifu, hupunguza mzigo wa virusi mwilini kwa zaidi ya mara 200.
Ni sawa na kusema inapunguza hadi kufikia karibu na sifuri,” inaeleza ripoti hiyo. Onyo la utafiti Pamoja na kwamba njia hii imeonekana kuwa nzuri katika kuzuia maambukizi, wataalamu hao wanasema ni hatari pale inapotumika vibaya. Hatari wanayoizungumzia ni kwa muathirika iwapo atatembea na mpenzi ambaye ni pia ni muathirika, lakini akawa hajatumia ARV au ametumia lakini siyo kwa kiwango ambacho VVU vimepunguzwa hadi kufikia karibu na sifuri.
Wataalamu hao wanasema iwapo muathirika atapata maambukizi mapya, atajiweka katika hatari ya kupata usugu kwa aina ya dawa anayotumia. Hata hivyo, wataalamu na watafiti mbalimbali wameelezea utafiti huo kuwa ni mafanikio mazuri katika kurahisisha njia ya chanjo kutoa kinga kwa waathirika na wale ambao hawajaambukizwa. Kwa sasa zipo aina nane za chanjo za Ukimwi duniani ambazo wataalamu wapo kwenye hatua mbalimbali za majaribio na wamekuwa wakizielezea kuwa zinatia matumaini.
CHANZO: Mwananchi (www.mwananchi.co.tz)