Serikali, sekta binafsi kushiriki ununua mazao

 Benjamin Sawe na Beatrice Mlyansi

Maelezo-Dodoma

SERIKALI itaendelea kushirikisha sekta binafsi ili kushiriki kununua kwa wingi mazao, kuyasindika na kuyasambaza kwa bei nafuu kwenye maeneo yenye upungufu.

 Akijibu swali Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango lililouliza serikali inampango gani madhubuti kurekebisha kupanda kwa bei za vyakula kuliko uwezo wa wananchi kiuchumi, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Lazaro Nyalandu amesema serikali itaendelea kutoa elimu kwa wakulima ili kutumia mfumo wa  stakabadhi ya mazao ghalani.

 Alisema mfumo huo utawezesha kuondokana na tabia ya kuuza mazao yote hasa ya chakula wakati wa msimu  mavuno na kusahau kujiwekea akiba kitu kinachosababisha kutokea kwa uhaba hali inayochangia kupanda kwa bei baada ya kumalizika kwa kipindi cha mavuno.

 Alitaja sababu nyingine ni pamoja na upatikanaji duni wa nishati, gharama kubwa za usafirishaji,miundombinu na teknolojia duni.

 Pia alizitaja sababu za nje ni ongezeko la bei ya mafuta ya petrol duniani,uharamia wa meli katika ghuba ya Somalia na machafuko ya kisiasa katika baadha ya nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi.

 Alifafanua kuwa ongezeko la mahitaji ya mazao ya kilimo duniani kutokana na kushuka kwa uzalishaji kulikosababishwa na janga la ukame, mafuriko na tetemeko la ardhi hivi karibuni nchini Japan vimechangia kuwepo kwa uhaba wa chakula na hivyo kusababisha kuongezeka kwa bei ya chakula nchini.

Nyalandu alitolea mfano wa bidhaa ya sukari kuwa Serikali imefanya majadiliano na wadau wa kuzalisha na kusambaza bidhaa hiyo nchini na kukubaliana kutangaza bei elekezi kwa kuzingatia gharama za uzalishaji na usambazaji.

 Alisema kwa kipindi cha mwezi wa kwanza bei ya sukari ilifika sh. 2500 kwa kilo katika baadha ya maeneo ambapo kwa kupitia makubaliano bei ya wastani ilishuka hadi kufikia wastani wa Sh. 1600 hadi elfu mbili kwa kilo kwa mwezi mei.

Aidha Serikali imetoa maelekezo kwa wakala wa hifadhi ya chakula kuuza kwa bei nafuu kwa wasambazaji sehemu ya mahindi yaliyohifadhiwa katika maghala ili kuziba pengo la upungufu katika soko kwa nia ya kumpunguzia mlaji makali ya bei.