
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mji Mpya wakiwa wamebeba miche ya miti wakielekea kuipanda katika maeneo mbalimbali shuleni hapo.
Na Dotto Mwaibale
SERIKALI imesema waathirika wa mafuriko ya mto Msimbazi walioondoka baada ya kupewa viwanja maeneo ya Mabwepande na kurudi eneo la Msimbazi watanyang’anywa viwanja hivyo.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Sadiki kwenye maadhimisho ya kilele cha wiki ya upandaji miti Mkoa wa Dar es Salaam yaliyofikia tamati leo kwa upandaji miti kwenye viwanja vya Shule ya Msingi ya Mji Mpya iliyopo Mabwepande ambapo Wilaya ya Kinondoni ilikuwa mwenyeji.
“Natoa maagizo kuwa wale wote waliopewa viwanja na serikali hapa Mabwepande ambao wameondoka viwanja vyao wanyang’anywe kwani ni wasariti na wale waliouziwa imekula kwao kwani serikali haiwatambui” alisema Sadiki.
Sadiki alitoa mwito kwa wananchi kubadilika kwa kuacha kutumia nishati ya miti na mkaa badala yake watumie gesi ambayo inapatikana kwa wingi kutokana na jitihada za serikali ili kulinda mazingira.
Aliongeza kuwa suala la upandaji miti ni endelevu hivyo kila mtu mahali alipo apande mti walau mmoja na kuitunza kwani miti ni uhai.
Meya wa Manispaa ya Kinondoni Yusuf Mwenda alisema Manispaa hiyo inabustani kubwa maeneo ya Kilongawima hivyo wanajipanga kuanzisha mashindano ya ukuzaji na upandaji wa miti kwa kata zake 34 na mshindi atapatiwa zawadi.
Katika hatua nyingine amesema halmshauri hiyo itawakopesha fedha wananchi waishio Mabwepande ambao waliathiriwa na mafuriko kwa ajili ya kukamilisha upatikanaji wa hati za umiliki wa viwanja vyao kabla ya mwezi wa sita badala ya kusubiri fedha kutoka ofisi ya Waziri Mkuu.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda alisema changamoto ya kukamilika kwa nyumba za askari polisi na kituo cha polisi katika eneo hilo itakwisha katika kipindi kifupi kijacho.