Serikali Kutenga Bilioni 30 kwa Miradi ya Vijana

Nembo ya Taifa la Tanzania


 
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali imelenga kupata sh. bilioni 30/- ili zitumike kuendeleza miradi ya vijana kwa nchi nzima kwa shughuli za uzalishaji. Alitoa kauli hiyo Agosti 31, 2013 wakati akizungumza na viongozi na wananchi wa wilaya ya Igunga, mkoani Tabora mara baada ya kupokea taarifa ya wilaya hiyo katika kijiji cha Simbo akiwa katika ziara fupi ya kukagua miradi ya uzalishaji inayofanywa na vijana mkoani humo.
 
Amesema aliomba ridhaa ya Rais Jakaya Kikwete fedha za uwezeshaji wananchi kiuchumi zilizokuwa zinatolewa kwa vikundi mbalimbili na watu binafsi, sasa hivi zitumike mahsusi kwa ajili ya kuendeleza vijana katika shughuli za uzalishaji mali.
 
“Nilimuomba Mheshimiwa Rais tupate sh. bilioni tano kutoka katika Mfuko wa Mabilioni ya JK kwa nia ya kuendeleza vijana. Alipoisikiliza dhana nzima, akasema atatupatia sh. bilioni 10/- ili ziwekezwe katika mabenki. Kiwango hicho sasa kitaweza kutupatia sh. bilioni 30/- ambazo zikizungushwa kwenye miradi kama hii, zitaleta mabadilko makubwa,” alisema Waziri Mkuu.
 
Alisema nia ya Serikali ni kuwawezesha vijana kwa sababu wanachangia asilimia kubwa ya nguvu kazi ya Taifa hili na kwamba wanakabiliwa na tatizo la kimfumo kutokana na elimu waliyoipata kwamba wakihitimu ni lazima wataajiriwa.
 
“Viongozi hawana budi kukubali na kutambua kwamba asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima wadogo na wao kama viongozi wanao wajibu wa kuwasadia kuondokana na umaskini uliowazunguka kwa kuangalia fursa walizonazo na jinsi ya kuzitumia ili waondokane na umaskini huo,” alisema.
 
Alisema katika semina elekezi ya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, kila mmoja alipewa jukumu la kuhakikisha wanasimamia uendelezaji wa vijana katika shughuli za uzalishaji mali lakini ni wachache waliothubutu na kulisimamia suala hilo.
 
Alipongeza uongozi wa mkoa na wilaya kwa kusimamia uanzishwaji wa miradi ya vijana ya waliohitimu Chuo Kikuu wa kikundi cha GIYA (wanaolima alizeti na vitunguu), KIVUKI (wanaofuga kuku wa chotara) na vikundi vingine vya kilimo katika mazao ya alizeti na mbogamboga.
 
“Binafsi nimefurahishwa na mlichoonyesha katika taarifa yenu kwani nilikutana na wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) walioamua kuanzisha umoja wao wa wahitimu (SUGECO) na kuunda vikundi zaidi ya 50. Kati ya hivi, vikundi 11 tayari vimeanza kazi, ni mwamko wa kutosha ambao unapaswa uenee nchini kote,” alisema.
 
“Vijana wa SUA, wa GAYI, KIVUKI na vingine kama hivyo ni chachu tosha kwa maendeleo ya kilimo na ufugaji hapa nchini. Hawa sasa ni walimu wazuri kwa wakulima wa kawaida. Hawa wamesoma na sasa wanatekeleza kwa vitendo kile walichojifunza,” alisisitiza.
 
Alisema miradi wanayoiendesha ni mashamba darasa tosha kwa wakulima na wafugaji wa kawaida waishio kwenye vijiji ambavyo miradi hiyo inafanyika na kwamba watakuwa na msaada mkubwa katika kuwasadia kitaalamu wanavijiji hao.
 
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu alikagua mashamba ya vijana ya kilimo cha vitunguu katika bwawa la Bulenya, kijiji cha Igogo na Kijiji cha Mwanzugi. Pia alizindua mradi wa mashine ya kukamua mafuta ya alizeti na mradi wa vijana wa usafirishaji katika kijiji cha Simbo wilayani Igunga.