Serikali kutekeleza Mpangokazi wa APRM

“Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Taarifa ya APRM kuhusu Tanzania ilipokelewa vizuri na Wakuu wa Nchi na Serikali wanaoshiriki Mpango wa Kujitathmini. Nchi yetu ilitajwa kuwa mfano wa kuigwa katika kudumisha amani, kujenga umoja, demokrasia na uhuru wa watu, muungano na utatuzi wa mi-gogoro ya ndani ya nchi.

Na Hassan Abbas, Dodoma

SERIKALI imeahidi kwa mara nyingine kuwa itatekeleza kivitendo Mpangokazi wa Kitaifa wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) unaolenga kufanyiakazi kasoro za kiutawala bora zilizobainishwa katika Ripoti iliyokamilishwa na taasisi hiyo.

Hayo yamo kwenye hotuba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe iliyosomwa mjini hapa.

Kwa mujibu wa Waziri Membe, Tanzania imefikia hatua nzuri katika utekelezaji wa APRM ambapo tayari Januari mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete aliitetea ripoti ya Tanzania mbele ya Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika zinazoshiriki katika APRM.

“Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Taarifa ya APRM kuhusu Tanzania ilipokelewa vizuri na Wakuu wa Nchi na Serikali wanaoshiriki Mpango wa Kujitathmini. Nchi yetu ilitajwa kuwa mfano wa kuigwa katika kudumisha amani, kujenga umoja, demokrasia na uhuru wa watu, muungano na utatuzi wa mi-gogoro ya ndani ya nchi.

“Vilevile, nchi yetu ilihimizwa kuzifanyiakazi changa-moto za migogoro ya wakulima na wafu-gaji, imani za kishirikina, kuhakikisha manufaa ya kukua kwa uchumi yanawafikia wananchi na kutoa elimu kwa umma kuhusu Mipango na Sera za Serikali,” alisema.

Waziri Membe alizitaja kazi zijazo za Mchakato wa APRM hapa nchini kuwa ni Serikali kuanza kazi ya kutekeleza maoni na mapendekezo ya  Ripoti ya APRM kwa kuingiza mapendekezo hayo katika Mipango ya Serikali.

“Baada ya ku-kamilika kwa tathmini ya awali ya nchi na taarifa kuwasilishwa kwa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika wanaoshiriki Mpango wa APRM, kwa sasa APRM Tanzania inatarajiwa ku-tekeleza kazi zifuatazo: kuingiza Mpangokazi wa Kitaifa wa APRM kwenye Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Mipango ya Muda wa Kati ya Wizara, Idara na Taasisi za Serikali katika maeneo mahsusi ya utawala bora yanayohitaji mabadiliko ya kisera, kisheria na ki-taasisi;

Alitaja kazi nyingine kuwa ni “Kuwafahamisha Wananchi kupitia pro-gramu mbalimbali kuhusu matokeo ya Taarifa ya Nchi ya Utawala Bora (Country Review Report – CRR); kufuatilia utekelezaji wa Mpangokazi wa kitaifa wa kuondoa changamoto za utawala bora zilizobainishwa;

Kuandaa taarifa za kila mwaka za utekelezaji wa hatua mbalimbali za kuondoa changamoto zilizojitokeza kwa ajili ya kuziwasilisha katika vikao vya Umoja wa Afrika vinavyohusu masuala ya APRM; na kufanya maandalizi ya kufanyika tathmini nyingine ya utawala bora nchini

APRM ni Mpango wa uliobuniwa na viongozi wa Nchi za Afrika miaka 10 iliyopita na taasisi hiyo kuanzishwa katika nchi mbalimbali za Afrika. Tanzania iliyojiunga na APRM mwaka 2006 kwa sasa ni miongoni mwa nchi 33 wanachma wa APRM kati ya 54 za Umoja wa Afrika (AU).

Tamko la Waziri Membe Bungeni pia ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Jakaya Kikwete kwa kiongozi wa Timu ya Wataalamu wa APRM kutoka AU waliokuja kuhakiki zoezi la Tanzania kujitathmini ambapo aliwaahidi Serikali yake kufanyiakazi mapendekezo yatakayotolewa.