WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali imeanza kushughulikia utaratibu wa kurejesha utoaji wa elimu ya kidato cha kwanza hadi kidato cha nne katika baadhi ya shule kongwe ili kurudisha ufaulu uliokuwepo na kuimarisha malezi ya watoto kuanzia elimu ya chini.
Amesema uamuzi huo unafuatia kaulimbiu ya kutaka kuwajengea wanafunzi maadili mema katika mazingira ya shule za sekondari tangu wanapoingia kidato cha kwanza badala ya mfumo wa sasa ambapo wanakuja kupata mafunzo hayo kidato cha tano na cha sita lakini wanakuwa hawajapata msingi imara tangu wakiwa wadogo.
Ametoa kauli hiyo Septemba 21, 2013 wakati akizungumza na mamia ya wanajumuiya waliohitimu katika shule hiyo (Alumnae), wanafunzi waliopo pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria sherehe za Jubilei ya miaka 50 ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Weruweru.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo, alikuwa akijibu maombi yaliyotolewa na Dk. Maria Kamm ambaye aliongoza shule hiyo kwa miaka 22 kuanzia mwaka 1970 hadi 1992, pamoja na wazungumzaji wengine katika sherehe hizo.
Alisema Serikali ilikwishatoa maelekezo kwa Makatibu Tawala wa Mikoa kwa ajili ya shule tano ambazo ziliondolewa madarasa ya kidato cha kwanza hadi cha nne na mojawapo ya shule hizo ni Sekondari ya Wasichana ya Weruweru.
“Taarifa za awali zinaonyesha kuwa Weruweru ina uwezo wa kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza wakati wale waliopo wakiendelea na masomo yao. Tatizo litakuwa ni kwamba hamtaweza kuanza na mchepuo zaidi ya mmoja,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema mbali ya kigezo hicho, Serikali iliangalia pia shule zinazotaka kurudishiwa mpango huo kama zina eneo la kutosha kuongeza majengo na ikabaini kuwa shile hiyo ya Weruweru inalo eneo la kutosha. “Jambo hili linawezekana, kwa hiyo tutaangalia taratibu zilizopo zikamilike mapema na shule hii ianze kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza, na mwaka unaofuata wa kidato cha pili hadi tukamilishe,” aliongeza.
Waziri Mkuu alisema uamuzi huo umelenga pia kutekeleza Ibara ya 85 ya Chama cha Mapinduzi ambayo inaelekeza kwamba udahili wa wanafunzi wa kike katika Vyuo Vikuu ufikie asilimia 40 ya wanafunzi wanaodahiliwa kila mwaka.
“Nia ya Serikali ni kuongeza udahili wa wanafunzi wa kike katika Vyuo Vikuu hadi kufikia asilimia 40. Lakini ili kufikia hapo ni lazima kuwe na idadi kubwa ya wanafunzi waliohitimu ili kupata mnyororo uliokamilika. Lazima kuwe na muendelezo wa wahitimu wengi zaidi,” alisema.
Alisema hivi sasa idadi ya wanafunzi katika shule za sekondari nchini kote ni 1,884,272 ambapo kati yao wasichana ni 873,799 sawa na asilimia 46.4 wakati wavulana ni 1,010,473 sawa na asilimia 53.6.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alibainisha kwamba Tanzania hivi sasa ina vyuo vikuu 45 (vya serikali ni 14 na biafsi ni 31) ambavyo vina wanachuo wapatao 166,484 wakiwemo wanawake 60,592 (sawa na asilimia 36.4) na wanaume 105,892 (sawa na asilimia 63.6).
Mapema, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bw. Philip Mulugo alisema Serikali iliondoa mfumo wa kidato cha kwanza hadi cha nne katika baadhi ya shule ili kukabiliana na hitaji la shule nyingi za kidato cha tano baada ya kuanzishwa kwa shule za kata ambazo nyingi zina kidato cha kwanza hadi cha nne tu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliahidi kuisaidia shule hiyo kufanya harambee ili iweze kutimiza ndoto yake ya kukusanya sh. milioni 500 za kufanya ukarabati wa majengo ya shule hiyo kongwe.
“Nimemwambia Mwalimu Mkuu pamoja na kamati ya harambee, andaeni mchanganuo juuya nini hasa mnataka kifanyike kwa ajili ya ukarabati. Onyesheni kila darasa, maabara ama bweni litagharimu kiasi gani. Onyesheni vipaumbele vyenu halafu mniletee. Mimi nitachukua fursa ya kuomba mtu mmoja mmoja kwa maandishi ili watusaidie kukamilisha kazi hii nzuri ambayo mmeianza,” alisema.
“Tujipange upya kuona tunataka Weruweru ya namna gani, tunataka shule hii iweje miaka 50 ijayo… hakuna kurudi nyuma katika hili mliloazimia kulifanya. Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, mmetoa wahitimu 12,757 kutoka shule hii. Hii si idadi ndogo. Ni lazima tuhakikishe sifa ya Weruweru haipotei lakini kikubwa ni kuazimia kwa pamoja kwamba tunataka Weruweru ibadilike irudie enzi zake ilipokuwa ikitamba na kutoa watoto wengi waliofaulu kwa alama za juu,” alisema.
Katika harambee ya papo kwa papo, Waziri Mku alifanikiwa kuchangisha sh. milioni 62.6/- zikiwa ni fedha taslimu na ahadi. Hata hivyo, wana Alumnae wa Weruweru walikuwa wamekwishakusanya michango mingine ya ahadi na fedha taslimu na kufanya jumla ya michango yote kufikia sh. milioni 104.6/-.
Baadhi wa wanafunzi waliohitimu katika shule hiyo ni Dk. Asha-Rose Migiro, Dk. Mary Nagu, Balozi Mwanaidi Maajar, Bi. Anna Kilango Malecela, Dk. Mwele Malecela, Dk. Hellen Kijo-Bisimba, Hajat Amina Mrisho na wengine wengi ambao wameshika nafasi mbalimbali za uongozi katika mashirika, taasisi na Serikalini.