KATIBU Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Injinia Joseph Nyamhanga ametambulisha utaratibu mpya utakaotumika kupunguza vikwazo visivyo vya kiforodha ili kurahisisha biashara na usafirishaji kwa magari makubwa yanayosafiri kwenda nje ya nchi.
Utaratibu huo unaotarajiwa kuanza Mei mwaka huu utawezesha magari yanayosafiri nje ya nchi kukagulia katika vituo visivyozidi vinne ili kupunguza muda wa safari kwa magari yaendayo nje ya nchi na kuvutia wasafirishaji kutumia bandari ya Dar es Salaam.
“Tumetayarisha stika zitakazobandikwa kwenye magari yanayokwenda nje ya nchi ambayo yatasimama na kukaguliwa katika vituo vitatu kwa magari yanayotumia barabara ya kanda ya kati na vinne kwa yanayotumia kanda ya Dar es Salaam yaani TANZAM,” alisema Eng. Nyamhanga.
Eng. Nyamhanga amevitaja vituo hivyo vya barabara ya ukanda wa kati kuwa ni Vigwaza mkoani Pwani, Manyoni mkoani Singida na Nyakanazi mkoani Kagera na kwa ukanda wa Dar es Salaam yaani barabara kuu ya TANZAM- Dar es salaam hadi Tunduma na Uyole hadi Kasumulu vitatumika vituo vine ambavyo ni Vigwaza mkoani Pwani, Mikumi mkoani Morogoro, Makambako mkoani Njombe na Mpemba mkoani Songwe.
Vituo hivyo vya ukaguzi wa pamoja vitakuwa na huduma ya Mizani, Vituo vya Polisi, Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA), na maeneo ya kupumzikia madereva wanaosafiri kwenda nje ya nchi. Katika hatua nyingine Eng. Nyamhanga amesema ili kurahisisha biashara ya usafirishaji kati ya Tanzania na Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Africa (SADC), na Jumuiya ya Soko la Pamoja kwa Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) Serikali inaendelea kutoa huduma za pamoja mipakani one stop border post inayolenga kurahisisha huduma za forodha,uhamiaji na usimamizi wa ubora wa bidhaa na huduma, ulinzi na usalama kwa kutoa huduma hizo upande mmoja wa mpaka kwa nchi mbili husika.
Vituo hivyo vinavyojengwa katika mipaka ya Holili, Namanga, Horohoro, Sirari, Mtukula, Rusumo, Kabanga, Tunduma na Kasumulu vitaimarisha huduma za forodha, uhamiaji ulinzi na usalama.