Serikali kupima utendaji wa ma-DC

*Warugenzi nao dawa jikoni

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda amesema Serikali inaandaa vigezo vipya vya kupima utendaji wa Wakuu wa Wilaya ili kuachana na vigezo vya zamani ambavyo havioneshi ufanisi wa kazi zao.

Pinda ametoa kauli hiyo jana mjini hapa wakati akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera mara baada ya kupokea taarifa ya wilaya hiyo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Anjelina Mabula.

Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Kagera alipokea taarifa hiyo katika shule ya sekondari ya Nyailigamba ambako alisema wakimaliza Wakuu wa Wilaya watakaofuata ni Wakurugenzi wa Halmashauri na Manispaa. 

“Vigezo vya sasa vinatumia mbinu za kizamani… nimeagiza viandaliwe vigezo vipyana tukiona kuna Mkuu wa Wilaya hafiti, tunamweleza kuwa kazi imekushinda, tupishe … vivyo hivyo itakuwa kwa Wakurugenzi wa Halmashauri na kada nyingine…“ alisema.

Katika hatua hiyo ya kuhimiza uwajibikaji kwa wananchi, Waziri Mkuu amewataka madiwani kuwa wakali na kuhoji taarifa za utekelezaji wa kazi kutoka kwa Wakurugenzi ili kuhakikisha yale yaliyopangwa yanatimizwa.

“Ninataka madiwani muwe wakali katika kusimamia rasilimali za Serikali…siyo kudai tu kanuni haziruhusu. Wekeni kanuni itakayoruhusu mpate muda wa kuanza maswali kwa Mkurugenzi kabla ya kuanza vikao,” alisema.

Alisema utaratibu huo hauna nia mbaya bali ni kuwapa madiwani fursa ya kupata taarifa sahihi ambazo wakati mwingine hawana muda wa kuuliza

katika vikao. “Pia inawapa fursa ya kujua utendaji wa Serikali na pia uwafanya Wakurugenzi kuona madiwani wanafuatilia,” alisisitiza.

“Diwani anaweza kuuliza endapo kuna barabara tuliipangia lakini haijatengenewa kwa miaka mitatu, na Mkurugenzi atoe majibu ili madiwani wote wasikie na ikifika muda ambao aliahidi kutekeleza na bado haujakamilika wambane.”

“Wakurugenzi ni watumishi wa umma na madiwani nao ni watumishi wa watu, ninawasihi Wakurugenzi wawe tayari kutoa majibu ili wapewe maswali japo wiki moja kabla na inabidi waende na wataalamu wakusaidia kutoa ufafanuzi pale inapobidi…ni jambo zuri na nia ya Serikali ni kuleta uwazi na uwajibikaji,” alisema.
                   
mwisho