WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali itaitisha kikao cha wadau mbalimbali kutoka taasisi za dini, mashirika yasiyo ya Kiserikali pamoja na vyama vya siasa ili kujadili mustakabali wa Taifa la Tanzania na hasa suala la amani na utulivu.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana mchana (Jumatano, Machi 20, 2013) wakati wa mahojiano maalum na kituo cha Redio Vatican kilichopo Vatican City, mjini Roma, Italia.
“Serikali inatarajia kuitisha kikao cha wadau wote kutoka vyama vya siasa, mashirika ya dini, NGOs, ili kutafakari nini kifanyike ambacho kitasaidia kuendeleza amani na utulivu… tutaitisha kikao hiki tarehe 4 Aprili,” alisema Waziri Mkuu wakati akihojiwa na Padri Richard Mjigwa, Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Akijibu swali kuhusu kuwepo kwa vurugu na mauaji ya viongozi wa kidini nchini Tanzania, Waziri Mkuu Pinda alisema Serikali imechukua hatua za kisheria kwa kufanya uchunguzi wa kina kwa kila eneo na baadhi ya wahusika kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Alisema kwamba juhudi kubwa bado zinaendelea kuwasaka wahusika wa mauaji ya Padre Evarist Mushi aliyeuawa Visiwani Zanzibar.
Akiwa katika studio hizo, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaeleza Watanzania waliko ughaibuni ambao wanaisikiliza redio Vatican kwa njia ya mtandao ama redio hatua ambayo mchakato wa uundaji katiba mpya imekwishafikia kwa sasa.
Alitumia nafasi hiyo kuwaomba Watanzania na watu wenye mapenzi mema washikamane na waendelee kumwombea Papa Francis wa Kwanza ili aweze kufanikisha kazi ambayo amepewa na Mwenyezi Mungu aikamilishe.
“Ninamshukuru Mungu kwa kumteua mtu anayeamini ataliongoza Kanisa Katoliki… atasaidia kuimarisha utangamano wa dunia nzima, tuendelee kumuombea akamilisha kazi kubwa aliyopewa na Mwenyezi Mungu,” alisema.
“Ujumbe alioutoa kwenye misa ya jana umenigusa sana na hasa msisitizo wake wa kutaka kila mmoja wetu aone atawasaidiaje watu maskini… watu wanaotengwa, watu wanaonyanyaswa na watu wanaonyanyapaliwa”, aliongeza.
Waziri Mkuu alikuja Roma, Italia kumwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwenye ibada maalum ya kumsimika Papa Francis iliyofanyika kwenye juzi (Jumanne, Machi 19, 2013) kwenye viwanja vya Kanisa Kuu la Mt. Petro mjini Vatican.
Waziri Mkuu alisema ameguswa mno na Papa Francis wa Kwanza kwani ni kiongozi ambaye ametoa changamoto ya kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea maskini na wote wanaoonewa ili waweze kuondokana na baa la umaskini.
Idhaa ya Kiswahili ya Redio Vatican iko kwenye studio ambayo ilikuwa ikitumiwa na Baba Mtakatifu, Yohane Paulo wa Pili kupeleka ujumbe kwa waumini wote ulimwenguni. Radio Vatican ambayo inaendesha idhaa za lugha nyingine kadhaa za kimataifa, ina wafanyakazi 500 na ina programu 45 zinazoandaliwa na redio hiyo.