Serikali Kujenga Reli ya Mtwara – Mbamba Bay

Treni ya abiria Tanzania

Treni ya abiria Tanzania


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ametangaza rasmi kuwa Serikali itajenga Reli ya kuunganisha Bandari ya Mtwara, Mkoa wa Mtwara na Bandari ya Mbamba Bay, Mkoa wa Ruvuma, ili kurahisisha uchukuzi wa mizigo mikubwa na mizito ya bidhaa na maliasili inayopatikana katika eneo hilo la kusini mwa Tanzania.

Aidha, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) imetangaza kuwa itagharimia ujenzi wa barabara ya lami kati ya Mbinga na Mbamba Bay katika Mkoa wa Ruvuma na hivyo kukamilisha ujenzi wa lami wa barabara ya ukanda wa Mtwara (Mtwara Corridor) kati ya Mtwara na Mbamba Bay yenye kiasi cha kilomita 823.

Ujenzi wa miradi hiyo mikubwa miwili umetangazwa, Julai 21, 2014, wakati Rais Kikwete alipofungua barabara ya lami kati ya Songea na Namtumbo lenye urefu wa kilomita 71.4 iliyogharimiwa na Serikali ya Marekani chini ya Mpango wa Millennium Challenge Corporation (MCC) na taasisi yake tanzu ya Millennium Challenge Account – Tanzania (MCA-T) kwa gharama ya shilingi bilioni 180.

Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa Rais Kikwete kufungua barabara mpya iliyojengwa kwa lami katika ziara yake ya siku sita katika Mkoa wa Ruvuma. Julai 19, 2014, Rais Kikwete alifungua rasmi barabara ya Mbinga – Songea katika sherehe iliyofanyika mjini Mbinga.

Katika sherehe iliyofanyika katika Kijiji cha Migelegele, kilomita tano kutoka mjini Namtumbo, Rais Kikwete pia amezindua ujenzi kwa kiwango cha lami cha barabara ya Namtumbo hadi Matemanga yenye urefu wa kilomita 128.9, inayogharimiwa kwa pamoja na AfDB, Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo la Japan la JICA na Serikali ya Tanzania. Barabara hiyo ni sehemu ya Barabara ya Songea hadi Tunduru.

Chini ya mpango wa kugharimia ujenzi wa barabara hiyo, AfDB itatoa asilimia 63.23 ya gharama zote, wakati Serikali ya Japan itagharimia asilimia 23 na Serikali ya Tanzania itagharimia asilimia 13.65. Tayari ujenzi wa barabara hiyo umeanza, kiasi cha miezi mitatu iliyopita, na umekamilika kwa asilimia nne na mkandarasi tayari amelipwa asilimia 15 ya malipo yote ambayo ni sawa na shilingi bilioni 8.1.

Akizungumza kwenye sherehe hiyo kubwa iliyohudhuriwa na mamia kwa mamia ya wananchi, Rais Kikwete amesema kuwa ni muhimu kwa Serikali kujenga reli kati ya Bandari ya Mtwara na Bandari ya Mbamba Bay ili kufungua zaidi ukanda wa Mtwara (Mtwara Corridor) na pia kuweza kubeba mizigo mikubwa na mizigo kutoka eneo hilo.

“Kwa mujibu wa mipango yetu, kuna wakati tutakuwa tunabeba tani milioni moja za chuma kutoka machimbo ya chuma ya Liganga, Mkoa wa Iringa, tani milioni moja ya makaa ya mawe kutoka machimbo ya makaa ya mawe ya Mchuchuma, Mkoa wa Iringa na tani milioni moja ya makaa ya mawe kutoka machimbo ya Ngaka, Mkoa wa Ruvuma”.

“Lazima tujenge reli kwa sababu bila kufanya hivyo, tutaharibu barabara zetu hizi, ambazo tunazijenga kwa gharama kubwa, katika muda mfupi na pia hatua hiyo itafungua sana eneo hilo la kusini mwa Tanzania,” amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete pia ametoa shukurani tele kwa Serikali za Marekani na Japan na AfDB kwa kuendelea kusaidia maendeleo ya Afrika kupitia ugharimiaji wa ujenzi wa barabara mbali mbali nchini.

Ameishukuru Serikali ya Marekani kwa kukubali kuipa Tanzania msaada mkubwa zaidi wa MCC kuliko uliotolewa kwa nchi nyingine yoyote duniani – dola za Marekani milioni 698, ambazo miongoni mwa mambo mengine umesaidia kujenga barabara za Tunduma-Sumbawanga, Tanga-Horohoro, Namtumbo-Mbinga na barabara za Pemba.

Amesema kuwa msaada huo wa Marekani pia umewezeshwa kusambazwa kwa umeme katika mikoa 10 ya Tanzania Bara, utandazaji wa nyaya za umeme za chini ya bahari kwenda Zanzibar na kuboreshwa kwa huduma za maji katika mikoa ya Morogoro na Dar es Salaam.

Akizungumza katika sherehe hiyo, Mkurugenzi Mkazi wa MCC nchini, Bwana Karl Fickenscher amesema kuwa imekuwa ni furaha kubwa kwa Marekani na wananchi wake kushirikiana na Watanzania katika kufanikisha miradi hiyo mikubwa chini ya MCC. Amesema kuwa kimsingi, awamu ya kwanza ya MCC imeisha, tena kwa mafanikio makubwa na kuwa sasa mchakato unaendelea wa kukubaliana na awamu ya pili ya MCC.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa AfDB katika Tanzania, Bibi Tonia Kandiero amesema kuwa Benki hiyo, ambayo imesaidia miradi mingi ya maendeleo katika Afrika, iko tayari kugharimia ujenzi wa barabara ya Mbinga-Mbamba Bay kwa kiwango cha lami ili kukamilisha barabara ya lami ya Mtwara Corridor. Amesema kuwa mpaka sasa AfDB wakati mwingine kwa kushirikiana na Serikali ya Japan, kupitia JICA, imegharimia ujenzi wa barabara za Iringa-Dodoma, Minjingu-Singida, Arusha-Namanga na Dodoma-Babati.