Na Magreth Kinabo – Maelezo
SERIKALI inaandaa mpango wa kutoa huduma za magonjwa yasiyopewa kipaumbele (NTD,s) kwa pamoja ili kuweza kufikia watu wengi kwa kupunguza gharama. Hayo yamasemwa leo na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Neema Rusibamayila wakati akifungua mkutano wa tatu wa wa siku tatu wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele leo unaoendelea kwenye hoteli ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam.
“Tumekutana na wadau mbalimbali katika mkutano huu lengo ni tunataka kuandaa mpango wa kutoa huduma na dawa kwa magonjwa yasiyopewa kipaumbele kwa pamoja badala ya ugonjwa mmoja pekee. Tunaweza kupata matokeo zaidi na kusaidia kuwafikia watu wengi kwa kuwa utarahisisha utendaji kazi, utoaji elimu na dawa,” alisema Dk. Neema.
Dk. Neema aliyataja magonjwa hayo kuwa ni Usubi, Trakoma, Kichocho, Minyoo, Mabusha na Matende. Aliongeza kuwa hivi sasa huduma hiyo imeweza kufikia wilaya 108 kati ya 160. Hivyo changamoto iliyopo ni kufikia mikoa saba.
Alisema mpango huo ulianza mwaka 2012 na unaendelea hadi mwaka 2017, ambapo mafanikio yameonekana mfano katika kupambana na ugonjwa wa usubi utafiti ulifanyika umeonesha kuwa kati ya wilaya tisa ni wilaya mbili ndizo zitaendelea kupatiwa dawa.
Naye Meneja Mpango wa Taifa wa Magonjwa yasiyopewa kipaumbele(NTD,s), Dk. Upendo Mwingira alisema changamoto nyingine iliyopo katika kubabiliana na magonjwa hayo ni baadhi ya jamii kuwa na uelewa mdogo juu ya magonjwa hayo ambayo dalili zake si rahisi kuonekana kwa macho kwani huonekana baada ya muda mrefu mfano Matende na Mabusha.
Alisema baadhi ya jamii huwa mwitiko mdogo wakati wa utoaji wa huduma, hivyo Dk. Upendo aliitaka jamii kujitokeza kwa wingi wakati wa utoaji wa huduma hizo. Alizitaja baadhi ya athari ya magonjwa hayo kuwa ni ulemavu wa kudumu na miongoni mwa sababu zinazochangia kuwepo kwa matataizo hayo ni umasikini.